Hospitali ya Aga Khan imetoa msaada wa vifaa tiba vya kuzuia ugonjwa wa Mpox, unaojulikana pia kama homa ya nyani, kwa Wilaya ya Rufiji mwishoni mwa wiki. Msaada huo una thamani ya zaidi ya shilingi milioni 200.
Akikabidhi vifaa hivyo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Hospitali ya Aga Khan, Juma Dossa alisema msaada huo ni sehemu ya jitihada za kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, katika kukabiliana na changamoto za afya kwa wananchi wa Rufiji.
Pia, Dossa aliitaka serikali isisite kutoa taarifa mapema kwa uongozi wa hospitali hiyo endapo kutakuwa na mahitaji ya msaada wa kiafya ili waweze kutoa msaada wao pale inapohitajika.
Kwa upande wake, Meneja wa Mradi, Theresia Mohere, alisema wamekabidhi suti maalum, barakoa za kisasa zaidi ya 27,000, pamoja na glovu zaidi ya 5,000.
Wakati wa hafla hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Mohamed Mchengerwa, alisisitiza kuwa mpaka sasa Tanzania ipo salama kwani hakuna kesi yoyote iliyoripotiwa kuhusu ugonjwa huo. Aidha, aliwaagiza wakuu wa Mikoa kuimarisha ulinzi kwenye mipaka na kuhakikisha vifaa vilivyotolewa vinasambazwa kwenye hospitali zilizopo mipakani ili kuongeza ulinzi.
Mbali na kutoa vifaa hivyo, Hospitali ya Aga Khan pia iliweka kambi ya siku mbili katika Hospitali ya Ikwiriri, ambapo walitoa huduma mbalimbali za afya kwa wananchi 600.
Theresia aliongeza kuwa idadi ya wananchi waliojitokeza kwa ajili ya uchunguzi wa afya ni wengi kuzidi malengo ya watu 600 waliojiwekea.
"Lengo lilikuwa kuhudumia watu 600 kwa siku mbili, lakini kwa siku moja tumehudumia watu 482, wakiwemo wanawake 302 na wanaume 180, hali inayonyesha kuzidi kiwango cha kuhudumia watu 600 ndani ya siku mbili," alisema Theresia.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.