Shule ya Msingi Nianjema, iliyopo katika Mtaa wa Nianjema ‘A’, Kata ya Nianjema, Wilaya ya Bagamoyo, imefanikiwa kukamilisha mradi wa ujenzi wa bweni la kisasa kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Akizungumza kuhusu mradi huo, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Mwalimu Renatus Kisenha, alisema gharama za utekelezaji wa mradi ni Shilingi 141,400,000.00 huku akibanisha Lengo kuu la mradi huo ni kuwawezesha wanafunzi wenye mahitaji maalum kujifunza katika mazingira salama, yenye staha na ushirikishwaji, sambamba na kuwajengea ujuzi wa maisha na kuondoa unyanyapaa wa kijamii wanaokutana nao majumbani na mitaani.
Aidha alisema Bweni hilo jipya, lina uwezo wa kuhudumia wanafunzi 80, na kusema kuwa ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za kuboresha miundombinu ya elimu jumuishi nchini.
Mwalimu Kisenha alisema kuwa fedha zote zilitumika kikamilifu katika ujenzi, uliotekelezwa kwa mfumo wa force account kwa kutumia mfumo wa kielektroniki wa manunuzi ya Serikali (NeST), ambapo kazi ilianza rasmi tarehe 1 Februari 2024 na kukamilika tarehe 15 Julai 2024/2025.
Kukamilika kwa mradi huo kunatarajiwa kuongeza usalama, faraja na ari ya kujifunza kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum, pamoja na kuchochea maendeleo ya elimu jumuishi katika Wilaya ya Bagamoyo.
Kwa niaba ya walimu, wazazi na wanafunzi, uongozi wa Shule ya Msingi Nianjema umetoa shukrani za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuona umuhimu wa mradi huu na kuhakikisha fedha za ujenzi zinapatikana kwa wakati. Pia wamemshukuru Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri, na wananchi wote walioshiriki kufanikisha mradi huu muhimu unaolenga kuinua maendeleo ya watoto wenye mahitaji maalum.
Kwa sasa shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 1,688, wakiwemo wavulana 813 na wasichana 875, wanaofundishwa na walimu 27 (wanaume 10 na wanawake 17). Kati yao, 65 ni wanafunzi wenye mahitaji maalum wanaonufaika na mazingira rafiki ya kujifunzia pamoja na huduma za malazi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.