Mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo amewaasa wananchi wa mkoa huo kuhakikisha kuwa wanashiriki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kuchagua viongozi bora watakaowaletea maendeleo kwenye maeneo yao.
Mhandisi Ndikilo aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara Mlandizi wilayani Kibaha kwenye muendelezo wa ziara yake ya kusikiliza kero na malalamiko.
“Mkichagua viongozi wasio na sifa za uongozi uliotukuka watarudisha nyuma jitihada za maendeleo, na suala la uchaguzi ni la kila raia aliyejiandikisha, nenda kashiriki usije kulalamika kuwa viongozi waliochaguliwa sio wazuri” alisisitiza Mhandisi Ndikilo.
Akifafanua juu ya maandalizi, Mhandisi Ndikilo Alifafanua kuwa taratibu zote zimekamilika ikiwa ni pamoja na uwepo wa fedha, vifaa na uteuzi wa wasimamizi wa uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Novemba 24 mwaka huu.
Aidha, Mhandisi Ndikilo ametahadharisha tabia ya baadhi ya wagombea kupenda kutoa rushwa na baadhi ya wapiga kura kupokea na akaeleza kuwa kufanya hivyo si tu kuwa ni kinyume cha sheria bali pia ni kujikosesha nafasi ya kujiletea maendeleo kwa kipindi cha miaka mitano.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.