Mkoa Pwani, umetekeleza wito wa serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Rais John Pombe Magufuli wa kujenga viwanda vya madawa na vifaa tibana Vitendanishi ambapo inatarajia kuwa na viwanda vitatu, hali ambayo itaondoa adha ya kuagiza madawa kutoka nje ya nchi , na imekemea tabia inayofanywa na baadhi ya wawekezaji ya kutoa ajira kwa watu kutoka nje ya nchi na kuwanyima fursa hiyo wananchi wa Pwani na Watanzania kwa ujumla
.
Akielezea masuala ya uwekezaji na ajira ,wakati wa ziara yake ya kutembelea viwanda mjini Kibaha ,Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe Mhandisi Evarist Ndikilo alisema Viwanda vya madawa vitawezesha kuokoa mamilioni ya fedha yaliyokuwa yakitumika kununulia madawa kutoka nchi za nje.
Alieleza kuwa viwanda vitatu vinavyojengwa Mkoani Pwani ni pamoja kiwanda cha Kairuki Pharmaceuticals Industry Ltd ,Zinga Pharmaceuticals ambacho kitajengwa kwa ubia na Israel na kipo mbioni kuanza kujengwa na kiwanda cha Bahari Pharmaceuticals .
“Tumeitikia wito wa Rais Dk.John Magufuli ,lakini pia tangu kipindi cha nyuma tumejipanga kujenga viwanda hivyo ,kupitia ziara hii tunawathibitishia wananchi tunaunga mkono kauli ya serikali yetu”alisema Mhandisi Ndikilo.
Pia alieleza kuwa ,zipo fursa mbalimbali za uwekezaji lakini vijana na wazawa wanashindwa kukimbilia fursa hizo.
Ndikilo alisema wazazi na vijana bado hawajatambua kujipanga kukuza elimu na ujuzi wao kwa ajili ya kujipatia ajira kirahisi na alitoa rai kwa wawekezaji ,kuacha kuwanyima ajira wazawa na watanzania ambao wanaujuzi na sifa za kufanya kazi .
” Haiwezekani tunajenga viwanda vingi lakini vijana ,waTanzania hasa kutoka Pwani hawanufaiki na ajira zinazopatikana, suala hili haikubaliki na sidhani kama Pwani ama Tanzania nzima haina wenye sifa na ujuzi unaotakiwa ,hivyo aliwataka wawekezaji hao watoe kipaumbele kwa watanzania wenye uwezo .
Ndikilo aliongeza kusema kuwa, amepokea taarifa ya ujenzi wa reli ya Standard Gauge eneo la Soga hawatoi ajira hata ya udereva jambo ambalo analichunguza na atakapopata uhakika watachukua hatua zinazostahili.
Aidha Mh Ndikilo alionyesha masikitiko makubwa kutokana na taarifa kuwa mkandarasi wa ujenzi wa kiwanda cha Kairuki Pharmaceutical Industry anaagiza vifaa vya ujenzi kama nondo kutoka Uturuki kwa madai kuwa nondo zinazozalishwa hapa nchini hazina ubora.
Ndikilo alisema kuwa vipo viwanda vinavyozalisha nondo zenye ubora mfano kiwanda cha Kiluwa Investment kilichopo Mkoani Pwani hivyo akawataka kuanzia sasa wanunue nondo katika viwanda vilivyop ndani ya nchi.
Nae mkurugenzi mtaalamu wa Kairuki Pharmaceuticals Mhandisi.Valency Assenga alisema ujenzi wa mradi huo ulianza Machi 10 mwaka huu na mkandarasi ni Petra Construction Ltd Ltd na unatarajiwa kumalizika Novemba 2018.
Alielezea kuwa kazi zote zinaendelea vizuri na zipo katika hatua ya awali ya ujenzi ambapo kazi hiyo inatarajiwa kugharimu jumla ya fedha za kitanzania shilingi bilioni 3.9 kwa awamu ya kwanza.
Mhandisi .Assenga alitaja changamoto zilizopo kuwa ni miundombinu ya barabara,mradi kusuasua kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha na ucheleweshwaji wa uunganishwaji wa umeme.
Katika Hatua nyingine nae Mkurugenzi wa halmashauri ya Mji Kibaha, Bi Jennifer Omolo akizungumzia suala la mipango miji alisema wameanza zoezi la kupima Mji muda mrefu na wanaendelea na zoezi hilo .
Pia aliwataka watu waache kujenga na kufanya biashara kiholela bila kupangwa ,na kuwashauri waone watalaamu wa mipango miji Ofisi ya Mkurugenzi ili kupewa maelekezo ya kupata vibali vya ujenzi .
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.