Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Dkt Dorothy Gwajima ametoa siku 30 kwa Katibu Tawala Mkoa wa Pwani Dkt Delphine Magere kusimamia kamati inayofuatilia mradi wa upanuzi uboreshaji wa hospitali ya Rufaa ya Tumbi iliyopo Kibaha Mkoani Pwani ambao.umekwama kwa miaka kumi sasa.
Dkt Gwajima alitoa agizo hilo Machi 4,2021 Mjini Kibaha alipofika kufuatilia utekelezaji wa maagizo yake aliyoyoyatoa Desemba 24, 2020 alipotembelea katika Hospitali ya Tumbi kukagua huduma zinazotolewa pamoja na upanuzi wa majengo ya mradi huo.
Miezi miwili iliyopita Waziri huyo alitoa maagizo kwa Katibu Tawala wa Mkoa huo baada ya kubaini mradi huo kukwama utekelezaji wake kwa muda mrefu huku fedha zilizotajwa awali zikiongezeka kutoka Bilion tano hadi 29.
" Leo nimepokea taarifa ya Katibu Tawala niliyomuelekeza kufuatilia na kufanya tathmini katika uboreshaji na upanuzi wa majengo haya ya Hospitali hii ya Tumbi, sasa natoa tena siku 30 ifanyike tathmini ya kina kwenye mradi huo baada ya hii ya awali kuonyesha mapungufu na hasara " alisema Dkt Gwajima.
Aidha alisema kuwa katika ripoti aliyokabidhiwa na Katibu Tawala ilionyesha upotevu wa Shilingi Bilion 1.6 pia mkanganyiko wa wakandarasi wawili katika mradi huo ambao ni Suma JKT na Must Construction bureau.
"Ifanyike tathmini ya kina kwa mradi mzima siku zisizozidi 30 rejeeni katika vipimo vya jengo zima, kamati pia ihakiki uhalali wa Shilingi Bilion 29 wakirejea mpango wa upanuzi wa majengo zibainishwe sababu za ongezeko za fedha hizo kutoka Shilingi abilion 5" alisisitiza.
Gwajima alisema katika taarifa ya upanuzi wa majengo hayo makadirio yaliyofanywa na Mkoa yalilenga kutumia Shilingi Bilion tano kabla ya Serikali kuonyesha nia ya kufanya upanuzi katika mradi huo ambapo mapendekezo yalielezwa kuwa ni Shilingi Bilion 29 badala ya ile ya awali kwa majengo hayo.
Nae Katibu Tawala Mkoa wa Pwani Dkt Delphine Magere alisema amekabidhi ripoti hiyo ambayo imeeleza namna fedha zilizotolewa na Serikali zilivyotumika na upotevu uliobainika.
Dkt Magere alisema Serikali na wadau wamechangia kiasi cha Shilingi Bilion 9.4 kwa ajili ya upanuzi wa majengo hayo na kwamba hadi sasa Shilingi Bilion 5.5 zimetumika.
Alisema katika fedha hizo zilizotumika hakuna uhalisia wa thamani ya fedha, na kwamba upotevu uliobainika ni upande wa sampuli ya vipimo na si mradi mzima.
" Ripoti ya awali tuliyoikabidhi imeonyesha malipo hewa ambayo hayakufuata taratibu, sasa tunakwenda kufanya tathmini kugusa mradi mzima na ripoti yetu itaonyesha uhalisia wa hasara iliyobainika, kwa siku 30 tulizopewa tutaweza kukamilisha kwani mapungufu mengi tumeahayabaini tutakamilisha kwa wakati" alisema Dkt Magere.
Mganga mkuu wa Mkoa wa Pwani Dkt Gunini Kamba alisema pamoja na kuchelewa kukamilika mradi huo lakini ulazima wa upanuzi bado upo.
Gunini alisema michoro ya awali ilishapitwa na wakati na kwamba itachorwa mipya na kwamba maboresho na upanuzi utakapokamilika huduma za kisasa zaidi zitatolewa katika Hospitali hiyo.
Msanifu wa Majengo wa Mkoa wa Pweani Paul Korosso alikiri kuwepo na mkanganyiko wa wakandarasi wawili katika mradi huo na kwamba jambo hilo litabainika zaidi katika tathmini itakayofanywa kwa siku siku 30.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.