Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. philip Mpango ametoa maagizo saba kwa wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala Tanzania bara yatakayowaongoza kusimamia na kutekeleza ipasavyo majukumu kuwahudumia wananchi katika maeneo yao.
Dkt. Mpango ametoa maagizo hayo leo Agosti 22, 2023 wakati akifungua mafunzo ya siku sita ya Uongozi kwa viongozi hao katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere iliyopo Kibaha kwamfipa mkoani Pwani.
Miongoni mwa maelekezo aliyoyatoa ni pamoja na Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa kuzingatia maadili na nidhamu ya Utumishi wa Umma katika maeneo ya kazi, ushirikishwaji na utatuzi wa kero zinazowakabili wananchi na kutoa mapendekezo juu ya mambo mbalimbali ambayo yanapaswa kurekebishwa na serikali.
“Jambo lingine la muhimu sana ni dhana ya usiri, kipindi hiki cha utandawazi ni muhimu kuwa makini na wasiri wa mambo ya serikali, tuzingatie hilo kwa ajili ya ulinzi na usalama wa nchi yetu na kuhakikisha tunaongeza umakini katika usimamizi wa rasilimali za umma na kutekeleza kikamilifu miradi ya maendeleo," amesema Dkt. Mpango.
Aidha amewataka viongozi hao kutoa elimu kwa watendaji wao kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa mazingira na vyanzo vya maji ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi sambamba na kutangaza fursa zitokanazo na uhifadhi, ikiwa ni pamoja na biashara ya hewa ya karbon na uchumi wa bluu.
“Jitahidini kuziwezesha sekta binafsi kwa kuweka mazingira yenye vivutio ili wawekezaji kama washirika muhimu kwenye suala zima la maendeleo waje kwa wingi kwenye maeneo yenu badala ya kuwahitaji kwenye uchangiaji wa shughuli zenu kama vile mwenge,” ameongeza Dkt Mpango.
Amesema, mafunzo hayo yatawasaidia viongozi hao kusimamia matumizi ya fedha, lakini pia kuwawezesha kuratibu upandishaji wa vyeo vya watumishi bila upendeleo na vile vile kujibu barua mbali mbali za wanachi na za viongozi kwa wakati.
Amewaeleza viongozi hao kushughulikia mapema changamoto zozote zinazojitokeza kwenye jamii na akawaasa kujitahidi kusoma na kuelewa ipasavyo nyaraka mbali mbali za Serikali, kama vile Ilani ya Chama cha Mapinduzi - CCM, Mpango Mkakati wa Maendeleo wa 2020/2025 pamoja na sheria mbali mbali za nchi huku akiwafahamisha kuwa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan anatambua uwepo wa viongozi hao kwenye mafunzo hayo na kuwa ndiye aliyetoa muongozo ili yafanyike.
Awali, akitolea ufafanuzi juu ya umuhimu wa mafunzo hayo kwa Wakuu wa Mikoa na makatibu Tawala wa Mikoa, Waziri wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa - TAMISEMI Angela Kairuki amesema yatasaidia kuongeza ubunifu na weledi katika kutekeleza majukumu yao.
Amesema jumla ya mada 20 ambazo zimesheheni masuala mbalimbali ya utumishi wa umma zitafundishwa na kwamba wakimaliza mafunzo hayo watakuwa na ujuzi na maarifa ya kutosha.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge ambaye ni mwenyeji wa viongozi hao katika Mkoa huo anashiriki kikamilifu mafunzo hayo kwa ajili ya kumuwezesha kusimamia kikamilifu majukumu yake na kuufanya mkoa wa Pwani kuendelea kuwa kinara wa uwekezaji katika sekta ya viwanda, biashara, kilimo na uvuvi.
Mafunzo kwa viongozi hao yatahitimishwa Agosti 27, 2023.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.