Naibu Waziri wa Maji, Mheshimiwa Mhandisi Kundo A. Mathew, amezindua mradi wa kisima chenye thamani ya shilingi milioni 65 katika kijiji cha Diazile, kata ya Msonga, wilayani Chalinze, mkoani Pwani. Mradi huu ni sehemu ya mpango wa kitaifa wa visima 900, unaotekelezwa nchi nzima, ambapo visima 40 vimepangwa kuchimbwa mkoani Pwani, na tayari 29 kati ya hivyo vimekamilika.
Mradi huu unatarajiwa kuzalisha lita 2,500 za maji kwa saa na utanufaisha zaidi ya wakazi 3,000 wa kata ya Msonga. Kukamilika kwake kumeondoa changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi, ambao hapo awali walilazimika kutembea umbali mrefu kutafuta maji.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mheshimiwa Kundo alisema, “Mpango wa Serikali ni kuhakikisha hakuna kijiji kitakachoshindwa kupata maji. Tutahakikisha wananchi wanapata maji safi na salama kwa matumizi ya kila siku, na hatutakubali mtu yeyote kuharibu miundombinu ya maji.”
Aidha, Waziri Kundo alimpongeza Shirika la Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kwa usimamizi bora wa miradi ya maji vijijini, akisema juhudi zao zimepunguza adha ya maji na kuimarisha utekelezaji wa sera ya Serikali ya kumtua ndoo mama kichwani.
Kwa upande wake, Meneja wa RUWASA Mkoa wa Pwani, Eng. Beatrice Kasimbazi, alieleza kuwa zaidi ya shilingi bilioni 2 zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa mpango wa visima 900 nchini kote. Mkoa wa Pwani umepewa visima 40, na visima 11 vilivyobaki viko katika hatua za mwisho za utekelezaji.
Mradi huu ni moja ya juhudi za Serikali kuunga mkono azma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama kwa urahisi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.