Mkoa wa Pwani umeelekeza Wakurugenzi wa Halmashauri kutozalisha madeni kwa wafanyakazi ambayo mara nyingi hutokana na uhamisho wa vituo vya kazi.
Hayo yalielezwa na Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Samweli Kolombo alipomwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge kwenye maadhimisho ya siku ya Wafanyakazi iliyofanyika Chalinze kimkoa na akabainisha kuwa Serikali Mkoani Pwani huo haitasita kuzichukulia hatua taasisi na mashirika binafsi yanayokiuka sheria za kazi.
Alisema kuwa waajiri wasiozingatia haki za Wafanyakazi wao wanakwenda kinyume na sheria za nchi wanawanyonya watumishi wao na hivyo Serika ya Mkoa huo haipo tayari kuwafumbia macho.
"Nimepata taarifa kuhusu baadhi ya Taasisi ambazo hazifuati sheria za kazi kwa watumishi wao, hilo halitafumbiwa macho, litafanyiwa kazi, Siyo leo unamhamisha Mfanyakazi kwenda kituo kipya cha kazi humpi pesa ya uhamisho, baada ya miaka kadhaa tena unamhamisha na kumpeleka kwenye kituo kingine napo haumlipi, huo sio utaratibu mzuri hivyo hakikisheni mnawalipa kwanza,"alisema kanali Kolombo.
Awali, katika risala yake katibu wa TUICO mkoa wa Pwani, Neema Wilbard alisema kuwa changamoto zinazowakabili wafanyakazi Mkoani humo ni nyingi na akataja baadhi kuwa ni kutoongezwa Mshahara kwa Wafanyakazi malipo ya muda wa ziada na makato makubwa ya kodi.
Aliongeza kuwa changamoto zingine ni baadhi ya waajiri na mashirika binafsi kukiuka sheria, kanuni na taratibu za ajira kwa wafanyakazi wao ikiwemo kutowapa mikataba ya kazi hivyo wakaiomba Serikali kuliangalia hilo ili kuinua uchumi wa wafanyakazi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.