Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo imefanikiwa kwa mara nyingine tena kupata hati safi (Unqualified Audit Opinion) kwa Mwaka wa fedha 2017/2018, ikiwa ni mara ya tatu mfululizo kwa Halmashauri ya Bagamoyo kupata hati safi.
Hayo yamesemwa na Mkaguzi Mkuu Mkoa wa Pwani Bi. Mwajuma Mohamedi alipokuwa anawasilisha taarifa ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika kikao maalumu cha Baraza la Madiwani wa halmashauri ya Bagamoyo.
Bi. Mwajuma ameleza kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, kwa mujibu wa Katiba ya mwaka 1977 (Rev 2005) ibara ya 143 na sheria ya ukaguzi wa umma namba 11 ya 2918 kifungu cha 10(1) ni jukumu la la Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali kufanya ukaguzi wa taarifa za mapato na matumizi ya fedha za umma Serikali Kuu,Serikali za Mitaa,Idara na mashirika ya umma.
Pia alisema kuwa , baada ya ukaguzi huo anatakiwa kutoa matokeo ya ukaguzi na mapendekezo kutokana na ukaguzi huo na hatua zinazotakiwa kuchukuliwa na menejimenti zilizopo kwa mujibu wa sheria.
"Katika ukaguzi uliofanyika kwa mwaka wa fedha 2017/2018, Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo imepata hati safi na kufanya halmashauri hii kuendelea kupata hati safi kwa miaka mitatu mfululizo, kwani kwa Mwaka 2017/2018, mwaka 2016/2017 na mwaka 2015/2016 Bagamoyo imepata hati safi ya Mkaguzi na mdhibiti Mkuu wa hesabu za Serikali (CAG)”.alisema Mwajuma.
Nae kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Theresia Mmbando akizungumza katika mkutano huo maalum wa baraza la Waheshimiwa Madiwani amesema, ni jambo la kujivunia kwa Halmashauri na Mkoa wa Pwani kwa Bagamoyo kupata hati safi kwa miaka mitatu mfululizo, na kusisitiza kwamba maelekezo na mapendekezo yaliyotolewa na Mkaaguzi na mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG) katika ripoti yake iliyowasilishwa katika mkutano huo, yafanyiwe kazi ili kuondoa kasoro ndogondogo zilizoonekana kipindi ukaguzi ulipofanyika, ili Halmashauri iendelee kupata hati safi miaka ijayo.
Pia ametumia fursa hiyo, kuwaasa Waheshimiwa Madiwani na Wataalam wa Halamshauri kuhakikisha wanasimamia vyema ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri na kuongeza ubunifu katika kuanzisha vyanzo vipya kwa kutilia mkazo uandishi wa maandiko ya miradi ya kimkakati inayofadhiliwa na Serikali kuu kwa sasa, itakayoisaidia Halmashauri kuongeza mapato yake ya ndani.
Akifunga Mkutano huo wa Baraza la Waheshimiwa madiwani, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo Mhe. Said Ngatipura amesema, watahakikisha wanasimamia mapendekezo yote yaliyotolewa kwenye ripoti ya Mkaguzi na mdhibiti Mkuu wa Serikali na kusimamia ukusanyaji wa mapato ili kuhakikisha Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo inaendelea kufanya vizuri.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.