Halmashauri za Mkoa wa Pwani zimetakiwa kuhakikisha zinatoa fursa kwa maofisa michezo na utamaduni kujiendeleza kielimu ili kuboresha taaluma zao waweze kuinua vipaji kwenye Halmashauri zao.
Aidha imewataka walimu kutumia taaluma zao kuendeleza sanaa utamaduni na michezo kwa wanafunzi mashuleni.
Hayo yalisemwa Mjini Kibaha na mwakilishi wa ofisa elimu mkoa wa Pwani Benjamin Majoya wakati wa kufunga michezo ya Umoja wa Michezo kwa Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA) mkoa wa Pwani kwenye uwanja wa Shirika la Elimu Kibaha (KEC) Tumbi.
Majoya alisema kuwa maofisa hao wapate fursa kujiendeleza kwenye vyuo vya michezo kikiwemo kile cha Malya kilichopo mkoani Mwanza na Taasisi ya Sanaa na utamaduni Bagamoyo (TASUBA).
"Halmashauri za wilaya ndani ya Mkoa ziwapeleke kuongeza taaluma kwenye vyuo husika na zisiwazuie wanapotaka kujiendeleza kwani michezo ni ajira,"alisema Majoya.
Alisema kuwa walimu wa Michezo mashuleni nao wanapaswa kuwafundisha wanafunzi kupitia taaluma zao ili kuwajengea msingi wa Michezo wanafunzi ili waje kuwa wanamichezo wazuri baadaye.
"Michezo inamfanya mwanafunzi anakuwa na utimamu wa akili na kufanya vizuri katika masomo yake hivyo kuna haja ya kuwaendeleza kimichezo ili waweze kujiletea maendeleo,"alisema Majoya.
Aidha alisema kuwa ili kupata wanamichezo wazuri waamuzi wa Michezo hiyo wanapaswa kutenda haki na kutokuwa na upendeleo ili wenye vipaji waweze kupata nafasi pia wajilinde na magonjwa ya COVID-19 na UKIMWI.
Awali akisoma risala ya mashindano hayo mwenyekiti wa maofisa elimu mkoa wa Pwani Omari Kombo alisema kuwa mashindano hayo ni ya 26 ambapo jumla ya wanafunzi zaidi ya 100 wamechaguliwa kuunda timu ya mkoa itakayokwenda mkoani Tabora kushindana kitaifa yatakayoanza Agosti 9 hadi 20.
Kombo alisema kuwa Mashindano hayo yalishirikisha wanamichezo zaidi 800 na walimu 50 baada ya kuteuliwa timu hiyo ya Mkoa itaingia kambini kwa muda wa siku nne.
Alisema kuwa mkoa una shule za Michezo kwa ajili ya kuendeleza michezo ambapo shule hizo zinasubiri kuwekewa vifaa vya michezo ili kuibua na kuendeleza michezo.
Kwa upande wake ofisa michezo wa mkoa wa Pwani Grace Bureta alisema kuwa wamejiandaa vema na wanauhakika wa kurudi na ushindi kutokana na vipaji walivyoonyesha wachezaji.
Bureta alisema kuwa safari hii wametumia wataalamu wa michezo kuchagua wanafunzi wenye vipaji hivyo wana uhakika timu iliyochaguliwa ni bora.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.