Shirika lisilo la kiserikali la Doris Mollel Foundation limetoa msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 30 kwa ajili ya watoto wanaozaliwa kabla ya muda (njiti) na wenye uzito pungufu katika Hospitali ya Wilaya ya Rufiji. Lengo la msaada huu ni kupunguza vifo vya watoto hao na watoto wachanga.
Akizungumza wakati wa kupokea msaada huo mwishoni mwa wiki, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa, aliwataka wadau mbalimbali kuendelea kujitokeza kusaidia wananchi kwani bado kuna uhitaji mkubwa wa vifaa tiba na huduma za kijamii.
Pia, Waziri Mchengerwa aliwahimiza wahudumu na madaktari kutoa huduma kwa weledi, bashasha, na kuwahudumia wananchi kwa huruma na ufanisi. "Sitaki kuona mwananchi yeyote akidharauliwa anapokuja kupata huduma. Wahudumieni kwa bashasha na huruma," alisema.
Waziri Mchengerwa aliongeza kuwa hatasita kuchukua hatua za kinidhamu kwa uzembe wowote wa makusudi utakaofanywa na watoa huduma, ambao unaweza kusababisha madhara kwa wananchi. "Nikisikia uzembe wa makusudi, nitaagiza hatua za kinidhamu zichukuliwe mara moja," alisisitiza.
Vilevile, aliagiza changamoto za kupandishwa madaraja kwa watumishi wa afya zishughulikiwe haraka ili kuboresha maslahi yao na kuongeza ari na weledi katika utendaji kazi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Doris Mollel Foundation, Bi. Doris Mollel, aliishukuru serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kujali na kutenga bajeti kwa ajili ya watoto wanaozaliwa kabla ya muda (njiti).
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.