Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema ipo haja ya kuhakiki kampuni yaliyowekeza katika mkoa huo ili kujiridhisha na wanapolipa kodi.
Aidha ailwataka Mamlaka ya Mapato TRA kwenda Viwandani kufuatilia ulipaji wa kodi na eneo ambalo wanalipia
Kwa mujibu wa Kunenge hali ya ukusanyaji wa kodi haiendani na uwekezaji uliofanyika katika mkoa wa Pwani hivyo kwa kufanya tathmini hiyo itabainisha tatizo lilipo.
Aliyasema hayo jana katika kikao kilichofanyika kwa lengo la kufanya tathminiya utekelezaji wa bajeti mwaka ya 2021/2022 na mkataba wa Lishe pamoja na miongozo ya Elimu na ukusanyaji wa mapato katika mkoa huo.
Kunenge alisema ili kukuza uchumi wa mkoa huo na kuleta mabadiliko ya kimaendeleo ni lazima kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato.
Awali akizungumza katika kikao hicho Katibu Tawala wa Wilaya ya Bagamoyo Kasilda Mgeni alisema yapo baadhi ya makampuni yanafanya shughuli zao katika Halmashauri ya Chalinze lakini kodi wanalipa mkoa mwingine.
Mgeni alisema baadhi ya makampuni hayo yamekuwa yakienda kulipa kodi mahali wanapoenda kupeleka bidhaa hizo.
"Serikali iingilie kati ili ushuru ukusanywe kwa usawa na maeneo haya makampuni yanapozalishia yanufaike badala ya utaratibu wa baadhi yao wanavyo fanya kwa sasa" alisema Mgeni.
Katibu Tawala huyo alisema barabara zinaharibika na Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (TARURA) hawana bajeti ya kutosha hivyo kodi hizo zikisimamiwa vizuri zitaondoa changamoto hizo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.