Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Suleiman Jafo ameupongeza Mkoa wa Pwani kwa kuweka kampeni ya upandaji miti ili kukabiliana na uharibifu wa mazingira.
Jafo aliyasema hayo jana kwenye shule ya sekondari Ruvu Mlandizi Wilayani Kibaha wakati akizundua Kampeni ya utunzaji mazingira na matumizi ya nishati mbadala kwa mkoa huo iliyoandaliwa na Taifa Gesi benki ya NMB Wakala wa Misitu Tanzania TFS na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani.
Alisema kuwa kwa kampeni hiyo kwani itasaidia kutunza mazingira pia utasaidia kutangaza teknolojia mbadala ya matumizi ya nishati mbadala baada ya kupunguza matumizi ya miti kama nishati kwa ajili ya kupikia na matumizi mengine ya binadamu ya kila siku.
Aidha alisema kuwa mkoa wa Pwani ni moja ya mikoa minne ambayo imeathirika kwa kiasi kikubwa na uharibifu wa mazingira lakini baada ya kupata maelekezo kutoka kwa Rais Dk Samia Suluhu Hassan ya kutaka mikoa hiyo iweke mipango ya kukabili hali hiyo mkoa umejiongeza kwa kuwa na kampeni hizo za kukabili changamoto za mazingira.
Awali akimkaribisha Waziri Jafo akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge Mkuu wa wilaya ya Kibaha Nickson John alisema kuwa mkoa umeweka mikakati mbalimbali ili kutunza mazingira ikiwa ni pamoja na kupanda miti million 13.5 lakini hadi sasa wameshapanda miti milioni 9.7 ikiwa ni zaidi ya asilimia 70 ya malengo ili kurejesha uoto wa asili.
Kunenge alisema kuwa lengo linguine ni kudhibiti matumizi ya mkaa ambao asilimia 70 ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wanatumia mkaa kutoka mkoa wa huo ambapo vijana wengi wamejiajiri kupitia matumizi ya nishati mkaa na mazao ya miti ambapo mkakati ni kupunguza vibali kwa asilimia 50 ya matumizi ya miti.
Alisema kuwa mikakati minne imewekwa ikiwa ni pamoja na usimamizi wa mazingira, upandaji wa miti, matumizi ya nishati mbadala na uchumi mbadala ambapo matumizi ya gesi yanapunguza asilimia 40 ya gharama ya fedha ikilinganishwa na mkaa na kuwapeleka vijana 5,000 viwanda.
Naye Mkurugenzi wa kampuni ya Taifa gesi Anjela Bhoke alisema kuwa kila mwaka hekari 400,000 za miti zinapotea kutokana na matumizi mbalimbali ya miti ambapo moja ya mikakati yao ni kujenga kiwanda cha kutengeneza mitungi ya gesi ambapo wako tayari kusambaza gesi majumbani na kwenye taasisi za umma.
Mwakilishi wa benki ya NMB ambaye ni meneja Kanda ya Dar es Salaam Seka Urio alisema kuwa wametenga kiasi cha shilingi milioni 470 kwa ajili ya shule zitakazopanda miti 2,000 na kuitunza kwa asilimia 80 ambapo itapatiwa milioni 50, huku mshindi wa pilia kwa kupanda miti 1,500 akipata milioni 30 akiitunza kwa asilimia 70 na watatu akipata milioni 20 kwa kupanda miti 1,000 itakayokuwa imetunzwa kwa asilimia 70.
Naye mwakilishi wa TFS Kanda ya Mashariki Shaban Kiula alisema kuwa wamaendaa miti milioni 1.5 kwenye Shamba la miti la Ruvu Kaskazini kwa ajili ya kupanda kwenye misitu iliyoharibiwa kutokana na uvunaji holela unaofanywa na watu kwa ajili ya matumizi mbalimbali yakiwemo ya kuni.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.