Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo, amesisitiza umuhimu wa Kongani ya Viwanda Kwala katika kukuza uchumi wa mkoa wa Pwani na taifa kwa ujumla, akisema kuwa miradi hii itazalisha ajira kwa maelfu ya vijana na kuongeza uzalishaji wa bidhaa nchini.
Akizungumza Julai 31, 2025, wakati wa uzinduzi wa Kongani ya Viwanda Kwala pamoja na Bandari Kavu ya Kwala na huduma ya usafirishaji wa mizigo kwa reli ya kisasa (SGR), Dkt. Jafo alisema kongani hiyo itajumuisha viwanda zaidi ya 200 na uwekezaji wa zaidi ya dola bilioni 3 za Kimarekani.
Aliongeza kuwa uzalishaji wa bidhaa za ujenzi umeongezeka mara mbili, na sasa Tanzania haitahitaji tena kuagiza bidhaa kama mabati, nondo, vioo, na saruji kutoka nje, jambo linaloleta akiba na kukuza viwanda vya ndani.
Dkt. Jafo alifafanua kuwa bidhaa zitakazozalishwa mwaka mzima zitakuwa na thamani ya hadi dola bilioni 6, ambapo bilioni 4 zitatumika kwa soko la ndani na bilioni 2 kwa ajili ya mauzo nje ya nchi, hatua itakayochochea ukuaji wa uchumi wa viwanda.
Waziri Jafo aliishukuru Serikali kwa kuwekeza katika miundombinu hii muhimu na kuahidi kuwa Wizara ya Viwanda na Biashara itaendelea kusimamia na kuendeleza maono ya Rais Samia ya kuifanya Tanzania kuwa taifa lenye viwanda imara na fursa nyingi za ajira kwa vijana.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.