Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dk.Selemani Jafo amewataka Watendaji wa Serikali wanaochelewesha nyaraka za uwekezaji kuacha kukwamisha juhudi za Rais Samia Suluh za kuongeza uwekezaji.
Dk.Jafo aliyasema hayo alipokuwa akifungua kongamano la Uwekezaji na biashara Mkoa wa Pwani lililofanyika katika Chuo cha Siasa cha Mwalimu Julius Nyerere kilichopo Kwamfipa Kibaha.
Alisema Serikali inapambana katika kuboresha mazingira ya uwekezaji kwa kuunganisha maji, barabara na umeme kwenye maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji.
"Rais ameitangaza nchi kila sehemu, lakini pia nchi imefunguliwa kwa kila sehem hivyo asitokee mtendaji akakwamisha hizi juhudi kwa kuchelewesha nyaraka" alisisitiza.
Dk Jafo pia amewataka wawekezaji waliowekeza Mkoa wa Pwani Kuhakikisha wanafungua ofisi na kulipa ushuru kwenye mkoa husika.
Alisema wapo wawekezaji wamewekeza katika mkoa wa Pwani lakini ushuru wanalipa walipofungulia ofisi zao ambapo ni Dar es Salam jambo ambalo linashusha mapato ya Halmashauri husika kushindwa kufanya maendeleo.
"Wawekezaji fungueni ofisi Pwani Wilaya ziweze kupata mapato na kufanya maendeleo kutokana na ushuru na kukuza pato la mkoa na Taifa kwa ujumla, sio mwekezaji amewekeza Pwani ofisi ipo Dar Es Salam na analipa ushuru huko utaratibu huo unakosesha mapato Halmshauri zetu" alisema.
Katika hatua nyingine Dk.Jafo alisema nchi inaendelea kujengwa katika amani na kwa utulivu lengo likiwa ni kuvutia wawekezaji.
Aidha Dk Jafo alisema kwasasa nchi imejipambanua kwa kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji na kufungua fursa kwa wawekezaji wa nje ya nchi kuja kuwekeza.
" Rais wetu Samia Suluhu Hassani ameitangaza nchi kila sehemu na sasa tunaona wawekezaji wanavyoongezeka mazingira yameboreshwa barabara zimejengwa, usafiri wa anga na nchi kavu na hii itarahisisha bidhaa zinazozalishwa zisafirishwe kwa urahisi" alisema.
Waziri huyo pia aliishauri Wizara ya Viwanda na Biashara kushirikiana na Mkoa wa Pwani kuandaa Maonesho haya kila Mwaka ili kutangaza mkoa huo na mikoa mingine ipate fursa ya kufika kujifunza.
"Wizara ya Viwanda na Biashara itangaze mkoa wa Pwani kama mkoa wa Maonyesho ya Viwanda iwe inafanyika kila mwaka na kongamano la uwekezaji kama hili mikoa mingine ije ijifunze na nchi itangazike" alisema.
Awali Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge alisema Mkoa huo unadhamira ya kuwa wa mfano katika sekta ya uwekezaji na kwamba kongamano hilo pamoja na maonyesho ya biashara vinafanyika ikiwa ni kutekeleza vipaumbele vya Rais Samia Suluhu Hassan.
Kunenge ameongeza Kongamano hilo limefanyika kwa lengo kupata ufumbuzi na suluhisho la kuongeza uwekezaji.
Ameeleza kuwa kwasasa mkoa huo una viwanda 1,460 vikubwa vikiwa 90 huku kukiwa na kongani 23 za viwanda na kwamba katika kongani ya Sino Tan ya kwala inatarajia kuwa na viwanda 350.
Mkurugenzi wa SinoTan Jensen Huang alisema kwasasa wanaendelea kuwashawishi wawekezaji kutoka nje ya nchi kufika kujenga viwanda katika kongani hiyo na kwamba itajengwa kwa awamu itakamilika kwa kipindi cha miaka mitano.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.