Mjumbe wa Kamati ya Sensa kitaifa ambae pia ni Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt.Selemani Jafo ametoa Rai kwa Wananchi kutowabughudhi makarani wa Sensa bali wawape ushirikiano ili kupata takwimu sahihi kwa maendeleo ya Taifa.
Hayo ameyasema leo Agosti 21 alipohamasisha wananchi katika Tamasha la uhamasishaji wa sensa lililoandaliwa na Mkoa wa Pwani na kufanyika wilayani Kisarawe.
Katika hotuba yake, Jafo aliwahamasisha wananchi kushiriki kwenye sensa tarehe 23 Agosti, 2023 na akawaasa kutoa ushirikiano wa kutosha ikiwa ni pamoja na kuandaa taarifa zao watakazozitoa kwa makarani wa Sensa watakaofika kwenye Kata zao.
Alisema kuwa Kamati ya Sensa kitaifa imeridhika na maandalizi ya vifaa na kwamba makarani zaidi ya 200,000 watapita ili kufanikisha shughuli ya Sensa itakayofanyika nchi zima.
"Hii ni Sensa ya sita ambapo ya mwaka huu itakuwa ya aina yake tofauti na zilizopita kwani hata matumizi ya teknolojia yatakuwa ya kisasa kurahisisha uhifadhi wa taarifa,” alifafanua Jafo.
Jafo alfafanua pia kuwa shughuli hiyo itaendelea kwa siku sita, hivyo akawasihi wananchi kuwa tayari kuhesabiwa.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Pwani Alhaj Abubakar Kunenge alitahadharisha kuwa Serikali ipo macho kwa wale watakaofanya uhalifu ama kutaka kuvuruga Zoezi la sensa na akasema watashughulikiwa Kisheria.
Kunenge alisema kuwa Sensa ni muhimu kwa maendeleo ya wilaya, mkoa na Taifa kujua takwimu halisi ya watu na makazi.
Sambamba na hayo, Kunenge alisema mkoa Umejiandaa vizuri na sasa umefikia asilimia 96 ya maandalizi ya shughuli hiyo
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.