Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imefanya ziara ya siku mbili mkoani Pwani kwa lengo la kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Katika siku ya kwanza ya ziara hiyo, tarehe 8 Februari 2025, kamati hiyo ilitembelea Halmashauri ya Mji wa Rufiji na kukagua miradi mbalimbali ya afya na elimu, ambapo iliipongeza kwa usimamizi mzuri na utekelezaji wake kwa viwango vya juu vilivyowekwa na Bunge.
Akitoa pongezi hizo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mheshimiwa Justine Nyamoga (Mb), alisema kuwa miradi inayotekelezwa Rufiji, ikiwemo ukarabati wa Hospitali ya Wilaya ya Rufiji na ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Bibi Titi Mohamed, imetekelezwa kwa ubora wa hali ya juu ukilinganisha na miradi mingine katika baadhi ya mikoa nchini.
Mwenyekiti huyo, akiwa ameambatana na wajumbe wa kamati, Naibu Waziri wa TAMISEMI, Mheshimiwa Zainab Katimba, pamoja na Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Mheshimiwa Rashid Mchatta, walitembelea na kukagua maendeleo ya miradi mbalimbali, ikiwemo ujenzi wa jengo la utawala, soko jipya, pamoja na shule maalum ya sayansi ya wasichana ya Bibi Titi Mohamed.
Tumekuja kukagua lakini pia tumejifunza mbinu bora za usimamizi wa miradi. Tumetembelea miji mingi kukagua miradi, lakini hapa Rufiji tumekutana na mfano mzuri wa usimamizi wenye viwango vya juu,†alisema Mheshimiwa Nyamoga.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa TAMISEMI, Mheshimiwa Zainab Katimba, alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutenga zaidi ya trilioni moja kuboresha huduma za afya, ambazo zimewezesha ujenzi wa zahanati, vituo vya afya, hospitali, pamoja na ununuzi wa vifaa tiba. Aliongeza kuwa katika sekta ya elimu, serikali imetenga zaidi ya trilioni 1.2 kwa ajili ya utekelezaji wa mpango wa BOOST,unaolenga kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani na kusaidia watoto wanaotembea umbali mrefu kufuata shule.
Aidha, Kamati ilihimiza kukamilishwa kwa haraka kwa baadhi ya miundombinu iliyopo katika hatua za mwisho, ikiwemo Mfumo wa Nishati Safi ya Kupikia katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Bibi Titi Mohamed, uwekaji wa mafeni katika bwalo la chakula, pamoja na ujenzi wa jengo la huduma ya mama na mtoto katika Hospitali ya Wilaya ya Rufiji.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.