Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imehitimisha ziara yake ya kikazi ya siku mbili mkoani Pwani kwa kutembelea miradi mbalimbali ya afya na elimu katika Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha.
Kamati hiyo ilikagua ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Mji Kibaha, Kituo cha Afya Pangani, Shule mpya ya Msingi Mtakuja, na Shule mpya ya Sekondari Tangini.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mheshimiwa Justine Nyamoga, akihitimisha ziara hiyo, alisema kuwa kamati kwa ujumla imeridhishwa na utekelezaji wa miradi kwa ngazi ya mkoa.
Alisisitiza kuwa miradi hiyo inatekelezwa kwa viwango vinavyokubalika, na kwamba kamati imejionea maendeleo mazuri yaliyofikiwa.
Aidha, kamati imeelekeza kuboreshwa kwa miundombinu ya maji, hasa vyooni, kuweka mazingira rafki kwa ajili ya watoto hasa wale wa awali pamoja na kuweka miundombinu sahihi kwa ajili ya watu wenye ulemavu.
Pia imehimiza kufuata kwa asilimia mia moja muongozo wa serikali katika utekelezaji wa miundombinu ya elimu ili kuhakikisha ubora na upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa TAMISEMI, Mheshimiwa Zainab Katimba, alikiri kupokea maelekezo hayo na kuhakikisha kwamba yatatekelezwa kwa umakini.
Alisema Serikali itafanya kazi kwa karibu na viongozi wa mikoa na halmashauri kuhakikisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo unafanyika kama ilivyoelekezwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.