Mikoa ya Pwani, Dar es salaam, Morogoro na Tanga inayounda Kanda ya Mashariki imedhamiria kuwa ya mfano katika Uwekezaji kutokana na uwepo wa fursa nyingi kwenye sekta za kilimo, mifugo na uvuvi nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya wakuu wa mikoa hiyo ijumaa Julai 28, 2024 kuhusu ufunguzi wa Maonesho ya Nane nane Kanda ya hiyo yatakayofanyika kwenye Viwanja vya nanenane mjini Morogoro kati ya Agosti 1-8 mwaka huu, Mkuu wa mkoa wa Pwani mhe.Abubakari Kunenge alieleza kuwa maonesho hayo yatakayofunguliwa na Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mizengo Kayanza Peter Pinda yana dhamira ya kuwezesha jamii kuongeza tija kutokana na maarifa mapya watakayoyapata ili kuinua sekta hizo kwa kutumia mbinu, mifumo na teknolojia mpya za kisasa.
Alisema, maonyesho hayo ni ya 30 tangu kuundwa kwa Kanda hiyo mwaka 1993 na kuwa mwaka huu wa 2023 wadau wamejitokeza kwa wingi na tayari 589 sawa na ongezeko la asilimia 22 kutoka wadau 476 wa mwaka 2022 wameshajisasijili kushiriki.
Kunenge alieleza kuwa, kauli mbinu ya mwaka huu inasema "Vijana na Wanawake ni Msingi imara wa Mifumo endelevu ya Chakula," kwani mchango wa vijana na wanawake unatambuliwa katika kuimarisha chakula na matumizi yake.
"Kauli mbinu hii inaendana na jitihada za Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, ambae anahimiza kuongeza uzalishaji wa chakula kulisha Bara letu na Dunia.
Kunenge aliwaomba wananchi wajitokeze kwa wingi katika maonesho hayo ili waweze kujionea teknolojia mbalimbali za kisasa zitakazowawezesha kuongeza uzalishaji na tija kupitia Ufugaji, Uvuvi na Kilimo.
"Kanda ya Mashariki ni ya kiuchumi, inayokuwa kwa kasi na mafanikio hayo yote yanawezekana, na yanaakisi matokeo ya kila siku na kuongeza tija," alifafanua Kunenge.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.