Katibu Tawala Msaidizi wa Idara ya Mipango, Bibi Edina Kataraiya, amezindua kikao cha kuratibu mafunzo kupitia Mradi wa Mwanamke na Ujuzi kwa Mama Vijana. Mradi huu unasimamiwa na Taasisi ya Anjita kwa kushirikiana na Serikali ya Mkoa wa Pwani.
Kikao hicho, kilichofanyika leo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, kimehusisha wanafunzi wa mafunzo hayo, Taasisi ya TAWAH inayotoa mafunzo, Shirika la Swiss Contact kama wafadhili wa mradi, wazazi wa wanafunzi, na baadhi ya watumishi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Mradi huu unalenga kuwapa ujuzi mama vijana 16 (waliozaa wakiwa na umri mdogo) katika fani ya ujenzi. Mafunzo hayo, yatakayoanza rasmi tarehe 20 Januari 2025, yatafanyika katika Chuo cha Mafunzo ya Ujenzi kilichopo Kijiji cha Muhaga, Wilaya ya Kisarawe, Mkoani Pwani.
Mafunzo hayo yatajumuisha hatua mbalimbali za ujenzi, kama vile Kuchanganya udongo na saruji, Kutafsiri michoro ya ujenzi, Kutengeneza matofali, Kupaua na kupaka rangi, Kuweka umeme katika nyumba, Kuchimba msingi, kuchanganya zege, na kujenga nyumba hadi kukamilika.
Akizungumza kwenye kikao hicho, Bibi Edina aliwasihi wanafunzi kusoma kwa bidii na kuwa na nidhamu, akibainisha kuwa mafunzo hayo ni fursa muhimu kwa maisha yao. Alisema:
“Mjione wenye bahati kwa kuwa masomo haya yanatolewa bure. Niwasihi msome kwa bidii, muwe na nidhamu, na tabia njema. Hii itawasaidia kujitegemea kiuchumi na kupata fursa zaidi kutoka kwa wafadhili.”
Aidha, aliwahamasisha kuwa mafunzo hayo ni suluhisho kwa changamoto zinazowakumba mama vijana. Aliongeza:
“Kuzalishwa siyo mwisho wa maisha. Kupitia mafunzo haya, tutapata ujuzi utakaotuwezesha kuanzisha biashara zetu na hata makampuni ya ujenzi.”
Kwa upande wake, Meneja wa Mradi wa Mwanamke na Ujuzi kutoka Swiss Contact, Bwana Helmani Nishani, alisisitiza kuwa mafunzo hayo yatatolewa bure bila gharama yoyote kwa wanafunzi.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Anjita, Bibi Janeth Mlale, alieleza kuwa taasisi hiyo kwa sasa ina zaidi ya wanafunzi 300 wanaoendelea na mafunzo katika fani mbalimbali, kama vile ushonaji, saluni, ufugaji, kilimo, uchakataji samaki, na uzalishaji wa mwani, katika Wilaya za Bagamoyo na Kibaha, Mkoani Pwani.
Mradi huu unatarajiwa kubadilisha maisha ya mama vijana kwa kuwapa ujuzi wa kujitegemea na kuchangia maendeleo ya jamii nzima.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.