Katibu Tawala Mkoa wa Pwani Mhandisi. Mwanasha Tumbo ameelekeza wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme chini ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuongeza kasi na kukamilisha miradi hiyo mapema ili kuwezesha wananchi kupata huduma ya Umeme kwa wakati.
Mhandisi Mwanasha ametoa maelekezo hayo leo Septemba 6, 2021 alipokuwa akizungumza na wajumbe wa Bodi ya REA Waliofika Mkoani hapo kwa Ziara ya Ukaguzi wa Miradi ya REA, Mhandisi Mwanasha amepokea taarifa ya maendeleo ya miradi pembezoni mwa Miji, Ujazilizi, na REA awamu ya tatu mzunguko wa kwanza mkoa wa Pwani.
“Kila mkandarasi afanye kazi usiku na mchana apunguze mda wa kutekeleza mradi, ongezeni vitendea kazi na watumishi ili kufanikisha azma ya Serikali ya Vijiji vyote kuwa na Umeme ifikapo 2022.” Alisisitiza Mhandisi. Mwanasha.
Alifafanua kuwa kwa sasa timu za wataalamu kutoka Ofisini kwake zinatembelea kila kata kwa Wilaya zote kufanya uhakiki wa utekelezaji miradi na kubaini changamoto zilizopo ikiwa ni pamoja na kubaini Vijiji vilivyokwishapata na ambavyo havijapata umeme.
“Baada ya kupokea taarifa ya timu hizo za ulezi, Mkuu wa Mkoa na mimi tutafanya ziara katika kila Kata kusikiliza changamoto zilizopo kwa lengo la kuzipatia ufumbuzi.” Alieleza Mhandisi Mwanasha.
Akiwasilisha taarifa hiyo, Mhandisi Thomas Mbaga aliyemuwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa REA alieleza kuwa wakandarasi wapo kwenye maeneo ya utekeleza miradi na yote inaendelea vizuri.
Wajumbe wa Bodi ya REA waliokuwa kwenye kikao hicho ni Louis Accaro na Dailin Mgweno ambao baadae walielekea Bagamoyo kukagua vifaa vya Mkandarasi Sengerema Eng. Co. Ltd.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.