Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete ameagiza takwimu za utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya za walengwa unaosimamiwa na TASAF ziakisi kila Halmashauri ili kupata tathmini sahihi itakayowezesha kujua uhitaji kwa usahihi.
Akizungumza na watendaji wa TASAF na wakuu wa idara wa Sekretareti ya Mkoa wa Pwani, Ridhiwani amehimiza taarifa zipatikane na kutolewa kwa kuzingatia hali halisi za wilaya ili kufikia malengo ya mradi.
Ameeleza kuwa malengo ya Serikali na Rais Samia Suluhu Hassan ni kuona milango inafunguliwa kwa walengwa kwa kubadilisha maisha yao na kuwatoa kwenye hali duni.
"Ziwepo taarifa zinazoakisi takwimu sahihi za wenye mahitaji kwa wilaya zote, hizi taarifa za kutoa kimkoa na wilaya moja moja tunakuwa hatupati tathmini kwa usahihi, Hatua hii itasaidia walengwa kujua idadi yao na kufikiwa ili kutimiza nia ya Serikali inayoelekeza kuwafikia kaya zenye watu wenye uhitaji," ameeleza Ridhiwani.
Katika kikao hicho, Katibu Tawala mkoa wa Pwani, Rashid Mchatta amesema kuwa mpango wa kunusuru kaya maskini unatekelezwa katika Halmashauri tisa zenye vijiji 417 na kuwa hadi kufikia Juni 2023 kaya zinazonufaika na mpango ni 35,427 idadi ambayo ameeleza kuwa imepungua kutoka kaya 37,663 kwa takwimu za mwaka 2020/2021.
Amefafanua kuwa upungufu huo umetokana na baadhi ya walengwa kufariki, kuhama, kufutwa katika mfumo na zingine kuhitimu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.