Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ismail Ussi, amewapongeza wakazi wa Wilaya ya Mkuranga kwa kuonyesha kwa vitendo namna wanavyomuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Akizungumza wakati wa mbio hizo, Ussi alisema hatua ya wananchi kutumia nishati safi siyo tu inaunga mkono jitihada za serikali, bali pia inalinda mazingira na afya za watumiaji.
“Nawaomba muendelee kutumia nishati safi kwa ajili ya kulinda afya zenu na mazingira. Viongozi wa Wilaya waendelee kushirikiana na wadau kuhakikisha kila kijiji na kata vinapata huduma ya nishati salama ya kupikia,” alisema Ussi.
Kwa upande wake, Meneja Mauzo wa Kampuni ya Puma Energy, Erick Meena, alisema kampuni hiyo inaunga mkono juhudi za serikali kwa kuhamasisha matumizi ya nishati safi miongoni mwa wananchi.
“Leo tumegawa mitungi 200 ya gesi kwa walimu wa Mkuranga. Lengo letu ni kuhakikisha kila mwananchi anatumia nishati safi ya kupikia, kuachana na matumizi ya kuni na mkaa ambayo yanaharibu mazingira na kuhatarisha afya,” alisema Meena.
Meena aliongeza kuwa matarajio ya kampuni yao ni kuona angalau asilimia 80 ya Watanzania wakitumia nishati safi katika maisha yao ya kila siku.
Katika ziara hiyo, Mwenge wa Uhuru umekagua, kuweka mawe ya msingi na kutembelea miradi sita ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 97 katika Wilaya ya Mkuranga.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.