Kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa, Amor Hamad Amor ameupongeza Mkoa wa Pwani kwa kusheheni viwanda mbalimbali na kuiomba jamii ivitumie kwa lengo la kujikwamua kiuchumi.
Aidha amewataka wawekezaji kutoa ajira pale inapostahili na kushiriki huduma za kijamii kwenye maeneo yao husika ili wananchi waweze kunufaika nao.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya Mwenge wa Uhuru kutoka Mkoani Pwani kwenda Mkoani Morogoro, eneo la Bwawani, Amor alisema wameagizwa kufanya kazi hivyo kwa Mkoa wa Pwani wameiona na wamefanyakazi .
Alieleza, Mkoa huu una viwanda vya kutosha ambapo vinaendana na dhamira ya Serikali ya awamu ya tano ya kuelekea kwenye uchumi wa viwanda.
"Tumejionea baadhi ya viwanda vinavyoendelea na ujenzi na vilivyokamilika ikiwemo kiwanda cha vipodozi, kiwanda kinachotengeneza dawa za viuadudu vya malaria, kiwanda cha kusindika matunda cha Sayona, pia vya kuchakata mihogo ,vya kutengeneza vigae ambavyo vyote vitasaidia kwa kiasi kikubwa kuinua mapato ya Halmashauri, Wilaya, Mkoa na Taifa" alisema Amor .
Amor, hakusita kuwataka vijana na makundi yote kufanya kazi na kuachana na tabia ya kukaa bila kazi kimazoea.
Alisema ni wakati wa kujiunga hata kimakundi kuanzisha viwanda vidogo na shughuli za kijasiriamali ili kujikomboa na hali ya umaskini.
Nae Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Eng. Evarist W. Ndikilo, akimkabidhi Mwenge wa Uhuru Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe Dkt. Kebwe Steven Kebwe, alisema Mkoa wake umejipanga kuwa ukanda wa viwanda kwani kitaifa kuna viwanda vikubwa 304 huku kimkoa vikiwa 84 na vilivobakia ndio mikoa mingine.
"Mkoa wa Pwani unatekeleza kwa vitendo ujumbe wa Mwenge wa Uhuru “Shiriki kukuza uchumi wa viwanda kwa maendeleo ya nchi yetu” ambapo kwa sasa una viwanda 264, Kati ya hivyo viwanda vikubwa ni 84 na vidogo 186 na kila Halmashauri imetenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji na kuna mazingira mazuri kwa wawekezaji,” alisema Mhe. Ndikilo.
Mhandisi Ndikilo, alipokea Mwenge wa Uhuru kutoka Dar es salaam, June mosi ambapo umetembelea halmashauri tisa, miradi 81 yenye thamani ya sh.bil 225.1. Kati ya miradi hiyo ,27 imewekewa mawe ya msingi, na miradi 27 imezinduliwa, miradi minne(4) imefunguliwa na miradi 25 imekaguliwa, miradi hiyo yote imechangiwa kwa pamoja na wananchi, Serikali Kuu, Halmashauri na wahisani wa ndani na nje .
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.