Kiongozi wa Mbio za Mwenge awataka Watanzania kudumisha amani kuelekea Uchaguzi Mkuu
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Ismail Ussi, amewataka Watanzania kudumisha amani na utulivu kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.
Hayo ameyanzungumza leo Aprili 5 wakati alipokuwa akiendesha mbio hizo katika Wilaya ya Rufiji, mkoani Pwani, Ussi aliwasihi wananchi kushiriki uchaguzi kwa njia ya amani na kuzingatia ujumbe wa Mwenge wa mwaka huu unaosema: “Jitokeze kushiriki Uchaguzi Mkuu 2025 kwa amani na utulivu.”
Mwenge wa Uhuru ulikagua, kuzindua na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo, pamoja na kuwasilisha ujumbe wa kitaifa wa Mbio za Mwenge kwa wananchi wa Rufiji.
Ussi alisema ameridhishwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo aliyokagua, na akawataka viongozi na wananchi kuhakikisha fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya miradi hiyo zinatumika kwa ufanisi na uadilifu.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Rufiji ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa, alisema Mbio za Mwenge zimeendelea kuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo kutokana na kufika kila pembe ya nchi.
Mchengerwa alieleza kuwa serikali itaendelea kupokea na kufanyia kazi maelekezo yanayotolewa na viongozi wa Mbio za Mwenge, sambamba na kuhakikisha wananchi wote wanashiriki kikamilifu katika maeneo yote ambayo mwenge unapita.
Aidha, aliipongeza Serikali kwa kuidhinisha fedha za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, hatua ambayo amesema imechochea kasi ya maendeleo ikilinganishwa na hali ya miaka 60 iliyopita.
“Katika kipindi cha hivi karibuni, Rufiji imepiga hatua kubwa katika sekta ya miundombinu, ujenzi wa shule na vituo vya afya. Shule zaidi ya 10 zimejengwa, na vituo vya afya vimeongezeka kutoka viwili hadi kufikia tisa,” alisema Mchengerwa.
Mwenge wa Uhuru umepitia jumla ya miradi sita ya maendeleo wilayani Rufiji, yenye thamani ya shilingi bilioni 1.6. Miongoni mwa miradi hiyo ni uzinduzi wa bweni katika Shule ya Sekondari ya Ikwiriri lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 80.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.