Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa Prof. Riziki shemdoe amezielekeza halmashauri zote nchini kuwekeza kwenye miradi yao ili iwasaidie kuongeza Mapato ya ndani kuwa endelevu.
Prof. Shemdoe ametoa maelekezo hayo Novemba 16, 2022 alipokuwa akikagua mradi wa Soko la Bwilingu wakati wa ziara yake ya kikazi kukagua miradi ya Maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze na kuridhishwa na ujenzi wa soko hilo lililojengwa kwa fedha zinazotokana na mapato ya ndani.
Akiwa katika ukaguzi wa Soko hilo, Profesa Shemdoe alikemea vikali tabia zinazofanywa na baadhi ya watendaji kuchukua vizimba na kuwakodisha wafanya biashara.
“Vizimba hivi vimejengwa kwa ajili ya wafanya biashara wa eneo hili, hivyo sitegemei kupata taarifa ya mtumishi yeyote kuchukua kizimba cha soko na kumpangisha mfanya biashara, hii miradi ni ya wananchi, waachieni kwani wao ndio wanufaika wa miradi hii,” alisema Prof. Shemdoe.
Aidha ameipongeza halmashauri hiyo kwa kuweza kufanya vizuri katika ukusanyaji wa Mapato kwani tokea halmashauri hiyo ianzishwe, mapato yake yamekuwa yakiongezeka kila mwaka.
Pia amezielekeza halmashauri kuwasikiliza wananchi katika kutatua kero mbalimbali zinazowakabili na akasisitiza Watumishi wa Halmashauri hiyo kuendelea kufanya kazi kwa weledi zaidi kwa kutoa huduma bora kwa wananchi na kuwaasa kuacha kufanyaiana Majungu Maofisini.
“Maofisini ndio sehemu ambayo mtu anakaa muda mrefu kuliko mahala kwingine, hivyo nawaomba tupendane na tuache kufanyiana fitina na majungu Maofisini,” alieleza Prof. Shemdoe.
Katika Ziara yake hiyo, Prof. Shemdoe pia alifanya ukaguzi wa ujenzi wa vyumba vya madarasa unaoendelea katika Halmashauri hiyo na ujenzi wa chumba cha dharura na cha upasuji katika Hospitali ya Msoga na akaridhishwa na hatua zilizofikiwa katika Miradi hiyo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.