Kiwanda cha kutengeneza nguzo za zege cha Hunnan Power, kilichopo mjini Kibaha Mkoani Pwani kimefungwa kutokana na kukosa na soko , tangu uzalishaji uanze mwezi septemba mwaka jana.
Kutokana na hali hiyo, kiwanda hicho kimebaki gofu na kupunguza ajira kutoka wafanyakazi 30 hadi wawili kwa sasa.
Hayo yalibainika wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani , Mhe.Mhandisi Evarist Ndikilo ,alipotembelea kiwanda hicho wakati wa ziara yake ya kutembelea viwanda vilivyopo mjini Kibaha.
Alisema Mkoa wa Pwani unadhamira ya kuwa ukanda wa Viwanda vinavyozalisha bidhaa mbalimbali lakini endapo soko litakuwa hakuna ,wawekezaji watakata tamaa na kufunga Viwanda vyao.
Pia aliongeza kuwa mkoa una viwanda vinavyotengeneza nguzo za zege viwili ikiwemo kiwanda cha Hunnan Power kilichopo mjini Kibaha na East Africa infrastructure engineering Ltd kilichopo Fukayosi Bagamoyo ambavyo vinahofiwa kushindwa kuendelea kuzalisha kwasababu ya bidhaa zake kukosa wateja.
“Katika ziara hii tumebaini changamoto ya kiwanda cha Hunnan Power kukosa masoko na zabuni kutoka shirika la umeme (Tanesco ),hawajapata zabuni kwa mara tatu .Hali hiyo imesababisha kiwanda hicho kufungwa, hakizalishi tena ,mashine zimefungiwa ndani ,kiwanda kimezungukwa na nyasi ,kimekuwa gofu na ajira hakuna, suala hili linaangusha juhudi za Rais Dkt John Pombe Magufuli ,Mkoa na Serikali”alisema Ndikilo.
Aidha Mhe. Ndikilo alieleza kwamba, wawekezaji wanajitoa kuunga mkono na kuitikia wito wa serikali wa kujenga viwanda lakini baadhi vinakumbana na changamoto ya ukosefu wa soko la uhakika.
Aliahidi kuzungumza na waziri mwenye dhamana ili kutatua tatizo hili na mkoa utafuatilia ili kuhakikisha unanusuru Viwanda vilivyokwisha anza kazi visifungwe.
Ndikilo aliitakaTanesco kuangalia kwa jicho la tatu tatizo hilo na kuangalia namna ya kutoa zabuni ili kuokoa viwanda hivyo.
Pia alitaja changamoto nyingine alizofikishiwa kwenye ziara hiyo,kuwa ni umeme,maji barabara na vibali kutoka TFDA.
Aliwasihi viongozi wa Wilaya na Halmashauri kuandika barua moja kwa moja kwa taasisi husika watatue matatizo hayo ili kuwavutia wawekezaji .
Awali akitoa taarifa ya kiwanda cha Hunnan Power, mkalimani wa kiwandani hapo, Suleiman Ramadhani alisema kiwanda kilianza ujenzi Jan 2017 na kuanza uzalishaji Septemba 2017 na kimegharimu dola milioni mbili za kimarekani na hakijawahi kuuza hata nguzo moja kwani Mpaka sasa hawajapata soko la Uhakika.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.