Kiwango cha Maambukizi ya Ugonjwa wa UKIMWI Mkoani Pwani kimeshuka kutoka asilimia 7.1kwa mwaka 2003 hadi asilimia 5.5 Mwaka 2017.
Hayo yalisemwa mjini Kibaha na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mh. Mhandisi Evarist Ndikilo wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kupima VVU na kuanza dawa mapema kwa wenye maambukizi Mkoa wa Pwani.
Ndikilo alisema kuwa katika kipindi hicho maambukizi yameshuka kutokana na mafanikio mazuri ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI Mkoani Pwani na nchini kwa Ujumla
"Kampeni hii ambayo imepewa jina la Furaha yangu – Pima, Jitambue - Ishi inatoa ujumbe wa furaha kwa wote wanaopima na kujua hali zao za maambukizi na kwa wale wanaokutwa nayo wanaanzishiwa matibabu tofauti na zamani mpaka kinga za mwili (CD4) zishuke," alisema Mhandisi Ndikilo.
Aidha alisema kuwa Tanzania ni kati ya nchi zinazoonyesha mafanikio katika mapambano dhidi ya maambukizi ya VVU kwa kiwango kikubwa.
"Tanzania imekuwa kati ya nchi zinazoonyesha mafanikio katika kupambana na maambukizi ya VVU kwa kiwango kikubwa.Takwimu za utafiti wa viashiria vya VVU na UKIMWI nchini kwa mwaka 2016-2017 unaonyesha kushuka kiwango cha maambukizi kutoka asilimia 7 mwaka 2003 hadi asilimia 4.7,"alisema Ndikilo.
Pia alisema kuwa hali ya kutojua hali zao za maambukizi ya VVU huleta athari kubwa kwa wenza na familia zao na inadhoofisha mapambano kwa Mkoa na nchi nzima kwa ujumla na zaidi kufikia malengo ya Millenia ya kupambana na ukimwi ya mwaka 2020 na 2030.
Mhandisi Ndikilo aliwataka watu wajitokeze kwa wingi kupima VVU ili kujua hali zao na wale wanaogundulika waanze dawa mapema na wasikubali kudanganyika kuacha dawa hizo mara afya zao zinapoonekana kuimarika.
Naye kaimu mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani Dk.Hussein Athuman alisema kuwa takwimu zinaonyesha kuwa jumla ya watu 307,486 sawa na asilimia 87 wamepatiwa huduma ya upimaji VVU kwa kipindi cha Januari hadi Septemba 2018.
Dk Athuman alisema idadi hiyo ni tofauti na mwaka 2017 waliopima walikuwa watu 189,005 kwa kipindi kama hicho.
Alisema kuwa changamoto waliyonayo ni kukosekana kwa mashine ya kupima wingi wa VVU na kulazimisha kutuma sampuli hospitali ya Lugalo hivyo kuchelewesha majibu na upungufu usioridhisha wa virusi katika kundi la watoto chini ya miaka 15 kutokana na ufuasi usioridhisha wa matumizi ya dawa.
" Huduma hizi zimefanyika kwa kushirikiana na Thps ambao wameimarisha huduma za upimaji katika Hospitali,vituo vya afya na zahanati kwenye mkoa wetu,"alisema Dk Athuman
Wadau ambao wameshiriki kwenye mapambano hayo ni Serikali ya Marekani kupitia mradi wa PEPFAR,mfuko wa dunia kupambana na Ukimwi,kifua kikuu na Malaria,asasi za kiraia za mapambano dhidi ya ukimwi THPS,ICAP,UMB,Pact-Kizazi kipya,Jsi,viongozi wa dini na vyama vya siasa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.