Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, ameifanya ziara ya siku moja jana katika Wilaya ya Rufiji na kukagua maendeleo ya ujenzi wa bwalo la chakula katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Bibi Titi na ujenzi wa Barabara ya Nyamwage-Utete. Ziara hiyo inalenga kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kwa viwango Bora.
Akiwa katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Bibi Titi, Kunenge amewataka wakandarasi kuongeza kasi ya ujenzi na kuhakikisha ubora unaozingatiwa. Ameeleza kuwa mkandarasi anatakiwa kumaliza ujenzi wa bwalo ifikapo Septemba 30, ili wanafunzi waanze kulitumia mara moja.
Ameagiza kuwa indaliwe ratiba upya pamoja na kuongeza wafanyakazi na kufanya Shughuli zaidi ya moja pale inavyowezekana ili kumaliza ujenzi kwa wakati.
Pia, ameagiza kwamba kama kuna changamoto za kiufundi, taarifa itolewe mapema ili kutafuta suluhisho.
Kunenge alisisitiza, "Tunataka bwalo hili likamilike kwa wakati. Tumewaambia wakandarasi waongeze kasi, kwani haturidhishwi na hali ya sasa. Tarehe 30 Septemba lazima iwe mwisho wa kazi."
Katika ukaguzi wa Barabara ya Nyamwage-Utete yenye urefu wa kilomita 33.7, inayojengwa kwa kiwango cha lami kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 43, Kunenge alionya kuwa mradi huo lazima ukamilike kwa wakati. Barabara hiyo inajengwa na mkandarasi M/s China Railway Seventh Group (CRSG), na mkuu wa mkoa aliwataka kuhakikisha ubora na muda wa mradi unazingatiwa ili kuepuka malalamiko kutoka kwa wananchi
"Ujenzi ukamilike kwa wakati nataka Mhe Rais wa Jamuhuri ya Mungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akija hapa wananchi waseme asante na sio kutoa malalamiko" alisema Kunenge.
Awali, Mhandisi Joseph Chuwa kutoka TANROADS alieleza kuwa mradi huo umefikia asilimia 5.01, sawa na thamani ya shilingi bilioni 1.9, huku miezi 14 ya utekelezaji ikiwa imepita.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.