Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge Ameupongeza Uongozi wa Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa huo - CORECU (1984) Ltd unao maliza muda wake kwa kuimarisha mnyororo wa thamani wa zao la Korosho na kuleta tija kwa wakulima.
Akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama hicho Jumanne April 30, 2024 kwenye Ukumbi wa Destiny Kibaha Kwa Matias, Kunenge ameeleza kuwa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita ubora wa korosho ulikuwa asilimia 12 na sasa umepanda kufikia asilimia 96.3.
Akitoa nasaha za kuwapata viongozi watakaoimarisha Ushirika huo katika uchaguzi wao, Kunenge amewaasa wajumbe kuwachagua viongozi wenye uwezo wa kupata majibu na kutafuta utatuzi wa changamoto za wakulima.
"Tutafutieni watu sahihi, tupate watu wenye uwezo wa kufanya mambo yakaonekana, chagueni watu safi," amesema.
Ameueleza mkutano huo kuwa Mkoa huo unafanya vizuri katika mambo mengi mbalimbali akitaja kwa uchache mafanikio katika lishe, elimu, Mwenge, mapato na viwanda, hivyo akawahamasisha kuhakikisha kuwa ushirika nao unaleta matokeo mazuri kama maeneo hayo mengine.
Mkuu huyo wa mkoa pia ameisisitiza CORECU kufanya kazi na taasisi za kitafiti ili kufanikisha malengo yao.
Wakati huo huo Mkuu huyo wa Mkoa amepokea msaada wa chakula (mchele tani 4 na maharage nusu tani) chenye thamani ya zaidi ya sh. Milioni 9 kutoka chama cha ushirika CHAURU ili kiwasaidie waliokumbwa na changamoto ya Mafuriko Rufiji na Kibiti Mkoani humo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.