Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mheshimiwa Abubakar Kunenge, ameongoza kikao kazi muhimu cha wataalamu kilicholenga kupokea na kupitia Taarifa ya Pato la Mkoa (GDP) pamoja na wasifu wa Mkoa huo.
Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani na kushirikisha wataalamu kutoka taasisi mbalimbali za umma na wadau wa maendeleo.
Akizungumza katika kikao hicho, Mheshimiwa Kunenge amesema kuwa Mkoa wa Pwani ni mkoa wa kimkakati unaochangia kwa kiasi kikubwa katika kukuza uchumi wa taifa kutokana na nafasi yake kijiografia na uwepo wa shughuli nyingi za kiuchumi.
“Mkoa wa Pwani una nafasi muhimu katika maendeleo ya kiuchumi ya nchi yetu. Hivyo ni lazima taarifa za pato la mkoa zitumike vizuri kupanga na kutekeleza mipango yenye tija,” alisisitiza Kunenge.
Katika kikao hicho, wataalamu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) waliwasilisha taarifa rasmi ya pato la Mkoa, ambayo ilijadiliwa kwa kina na kupokelewa na wajumbe wa kikao hicho.
Aidha, katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa ametoa wito kwa wataalamu wa uchumi kutoka Sekretarieti ya Mkoa na Halmashauri zote kufanya kazi kwa weledi, kushirikiana kwa karibu, na kuimarisha shughuli za utafiti na maendeleo (R&D), ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi. Pia amesisitiza umuhimu wa kuwapatia watumishi vifaa stahiki na mafunzo ya kuwawezesha kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Maafisa Mipango wa Halmashauri, wawakilishi wa benki, pamoja na Wakuu wa Taasisi mbalimbali za Umma kutoka Mkoa wa Pwani.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.