Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mheshimiwa Abubakar Kunenge, amewataka wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kisarawe na Shule ya Msingi Madubwike kuwekeza zaidi katika elimu ili kufanikisha ndoto zao, kupata nafasi za uongozi siku za usoni, na kuinua hali ya maisha ya familia zao kiuchumi.
Mheshimiwa Kunenge alitoa wito huo leo wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa ujenzi wa bweni katika Shule ya Sekondari Kisarawe, pamoja na ujenzi wa Shule ya Msingi na Shule ya Awali ya Madubwike, zilizopo wilayani Kisarawe, mkoani Pwani.
Alibainisha kuwa katika kipindi cha uongozi wa Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya elimu na kujenga shule mpya. Kwa Mkoa wa Pwani pekee, shule 42 za sekondari na 48 za msingi zimejengwa ili kuboresha upatikanaji wa elimu.
Mhe. Rais anataka watoto wasome, ndiyo maana Serikali inaendelea kuboresha na kujenga miundombinu ya elimu. Urithi bora kabisa kwa mtoto ni elimu,†alisema Mheshimiwa Kunenge.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa bidii na kujituma katika masomo, akieleza kuwa mafanikio ya wanafunzi yanategemea juhudi zao katika kujifunza na kutumia elimu kusaidia jamii na familia zao.
Hakuna mtu asiye na akili. Sote tuna uwezo wa kujifunza na kuelewa mambo muhimu kwa familia na taifa letu. Viongozi, akiwemo Mheshimiwa Rais, pamoja na wazazi wenu, wanajitahidi kuhakikisha mnasoma, hivyo mnapaswa kuwaheshimu na kutimiza wajibu wenu,†aliongeza Kunenge.
Pamoja na hayo, Mkuu wa Mkoa aliwahamasisha viongozi na wananchi kushiriki kikamilifu katika maandalizi ya Mbio za Mwenge wa Uhuru, ambapo uzinduzi wake utafanyika Aprili 2, 2025, katika Viwanja vya Shirika la Elimu Kibaha, wilayani Kibaha, mkoani Pwani.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.