Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amezielekeza Mamlaka za Serikali za Mitaa mkoani humo kuandaa mipango yenye tija inayoweza kuongeza mapato, huduma za jamii na kutatua kero za wananchi sambamba na kutozalisha hoja za Ukaguzi.
Akishiriki kwa nyakati tofauti Juni 16, 2025 katika vikao vya Mabaraza Maalum ya Halmashauri za Kibaha Mji na Halmshauri ya Wilaya ya Kibaha yanayojadili ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Mwaka 2023/2024, kunenge ameeleza kuwa hati safi inapatikana kutokana na utaalamu wa kuandaa mahesabu kwa mujibu wa taratibu na kanuni za fedha hata kama hakuna tija.
Akiwa katika Halmashauri ya Mji Kibaha, Kunenge alisema kuwa la msingi ni tija inayopatikana kwenye maandalizi ya nini kinachotakiwa kutumia fedha na kwamba kinyume chake halmashauri zinaweza kuelekeza fedha zikalipa kwa kitu ambacho ukiangalia hakina umuhimu lakini taratibu za malipo zikafuatwa na kupatikana kwa hati safi bilaya kuwa na tija.
"Ukiangalia katika mfumo mzima wa kupanga na usimamizi wa matumizi "Planning and Management System" unaangalia kipaumbele ni nini, unaangalia asilimia 20 inayokupa asilimia 80 ya matokeo unayoyataka, hicho ndiyo kigezo unachoangalia ndio unaangalia shughuli gani utafanya kisha unafikiria ufanye nini ili upate matokeo unayohitaji na kuyapanga kwa vipaumbele na kuyawekea thamani ya fedha, unaandaa na kuomba fedha hiyo kwenye Kamati ya Bunge mkishapewa mnasimamia matumizi yake ambayo yatakaghuliwa na CAG." Alisema Kunenge.
Amesisitiza kuwa iwapo matumizi yatawekwa kwenye mambo ambayo siyo kipaumbele hati safi itapatikana lakini hakutakuwa na tija.
Ameongeza kuwa suala la kufunga hoja nalo halina tija na akaeleza kuwa shida ni kwanini hoja zinatokea huku akisema kuwa kama zinaweza kufungwa kumbe pia zinaweza kuzuia zisitokee kabisa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.