Mkoa wa Pwani umeanza kutoa mafunzo ya matumizi ya mfumo mpya wa Manunuzi wa NeST kwa maafisa wa Mkoa, makatibu Tawala wa Wilaya na maafisa wa halmashauri zote za Mkoa huo nchini kwa lengo la kuutumia na kudhibiti mianya ya upotevu wa fedha pamoja na kuepukana na hoja za Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali CAG ambazo zimekuwa zikijirudia kila mwaka kuhusu upotevu wa fedha kwenye manunuzi.
Akifungua mafunzo hayo kwa maafisa washiriki leo Agosti 29,2023 kwenye ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Kaimu Tawala wa mkoa huo, Savera Salvatory, amesema mfumo huo mpya ni mbadala wa uliokuwa unatumika awali wa TANePS ambao ulikuwa na dosari nyingi ikiwa ni pamoja na kusababisha upotevu wa fedha za umma.
Amesema mfumo huo mpya umejengwa na kusimamiwa na watanzania wenyewe na kwamba utapunguza changamoto nyingi na utaondoa kazi kubwa kwa maafisa manunuzi kwa sababu mchakato wa manunuzi utaanzia kwa mtumiaji kwenye Idara au kitengo husika.
“Lengo la mfumo huu ni kuboresha na kudhibiti taratibu zote za manunuzi na kumrahisishia mtumiaji wa mfumo, ubunifu wa mfumo umetokana na kuwepo kwa changamoto mbalimbali na zingine tumezishuhudia kupitia taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali CAG hoja zikiwa zinajirudia katika mfumo wa awali wa TANePS,” amesema Savera.
Ameongeza kuwa miongoni mwa hoja za CAG ambazo zimekuwa zikijirudia kutokana na mfumo wa TANePS ni manunuzi yasiyoingizwa katika vitabu mbalimbali, manunuzi yaliyofanyika nje ya bajeti, manunuzi yasiyo na tija kwa serikali na taratibu ndefu za manunuzi kupitia mfumo huo.
Amesisitiza kuwa mfumo huo utaanza kutumika rasmi Oktoba mosi mwaka huu ambapo taratibu zote za manunuzi zitafanywa kwa njia hiyo kuanzia uandaaji wa mahitaji ya Idara husika uanzishaji wa tenda, uthamini, utoaji wa tenda na mahojiano.
“Mfumo huu mpya umeanza kutumika Julai mosi na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi Serikalini (PPRA) na kwamba imetoa muda wa miezi mitatu hadi Oktoba mosi mwaka huu 2023 mamlaka zote kuanza kutumia mfumo wa NeST,”amefafanua Savera.
Aidha, amesema baada ya Oktoba mosi kwa yeyote atakayebainika kutotumia mfumo huo hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa Afisa Masuuli wa Taasisi ambayo haitatumia mfumo huo kupitia kifungu namba 104 (2) (d) cha sheria ya ununuzi wa umma ambacho kinatoa adhabu ya faini ya sh milioni 10 kutoka mfukoni mwa Afisa Masuuli atakayekiuka sheria hiyo.
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi mkoa wa Pwani, Beda Mmbaga amesema jumla ya watumishi 104 wanapatiwa mafunzo ya matumizi ya mfumo huo mpya na kwamba elimu hiyo itatolewa mpaka ngazi ya chini ili kuhakilisha mkoa huo unaondokana na hoja za CAG kuhusu upotevu wa fedha za umma ambao unaripotiwa kila mwaka.
Amesema idadi hiyo ya watumishi 104 ni kubwa ukilinganisha na mikoa mingine na kwamba wamefanya hivyo mahsusi kwa kuwa mkoa huo ni wa kimkakati na wa viwanda hivyo watasaidia kuongeza ufanisi kwenye utendaji wa kazi zao.
Mshiriki wa mafunzo hayo Epiphanus Marcel ambaye ni Afisa Mkaguzi wa ndani Mwandamizi mkoani humo, amesema mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka kwani yatarahisisha utendaji kazi wao katika ufuatiliaji wa matumizi ya fedha na kuwa utawadhibiti baadhi ya watumishi wasiokuwa waadilifu kutumia dosari za mfumo wa awali kufuja fedha za umma.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.