Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutambua umuhimu wa afya kwa Watanzania, hasa kupitia mpango wa kupeleka huduma za kibingwa kwenye mikoa na halmashauri zote nchini (Bingwa Bobezi).
Kunenge alitoa shukrani hizo leo wakati wa hafla fupi ya kuwapokea madaktari bingwa 63 iliyofanyika ofisini kwake. Madaktari hao watatoa huduma za kibingwa kwa halmashauri zote tisa za Mkoa wa Pwani kwa muda wa siku saba, kuanzia tarehe 14 hadi 20 Oktoba. Kila halmashauri itapokea wataalamu sita kutoka fani tofauti, isipokuwa Halmashauri ya Mji wa Kibaha ambayo itapokea wataalamu saba, akiwemo mbobezi wa mifupa.
Aidha, Kunenge alimwagiza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Dkt. Kusirye Ukio, kutumia fursa hii kutathmini mahitaji makubwa ya huduma za afya ili kurahisisha ununuzi wa vifaa tiba muhimu, na kujua changamoto kubwa zinazowakabili wananchi wa mkoa huo katika suala la afya. Hatua hii itasaidia kuweka mipango thabiti ya kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
Kwa upande wake, Dkt. Kusirye Ukio alisema ujio huu wa madaktari bingwa ni wa awamu ya pili, ambapo awamu ya kwanza iliweza kuhudumia wananchi 2,517 wenye matatizo mbalimbali. Awamu hii ya pili itahusisha wataalamu mabingwa wa upasuaji wa mfumo wa mkojo, magonjwa ya kina mama na afya ya uzazi, upasuaji, afya ya kinywa na meno, usingizi, na mifupa.
Aliongeza kuwa lengo kuu la kupeleka wataalamu hao ni kuimarisha afya za Watanzania kwa kuwapatia matibabu ya kibingwa, na pia kuhakikisha watumishi wa vituo vya afya vya msingi wanapata mafunzo na uzoefu kutoka kwa mabingwa hao. Hii itasaidia kuboresha huduma na kupunguza rufaa ambazo zinaweza kushughulikiwa kwenye vituo vya afya vya mkoa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.