Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani na Skauti Mkuu wa Tanzania, Rashid Mchatta, amesema kuwa mafunzo ya utawala bora yatawasaidia wananchi kuelewa haki na wajibu wao katika jamii, pamoja na kuwajengea uwezo watumishi wa serikali katika kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Akizungumza Machi 14, 2025, na waandishi wa habari wilayani Kibiti, wakati wa mafunzo hayo kwa Wilaya za Mkuranga, Rufiji na Kibiti, Mchatta alieleza kuwa mafunzo haya yanatoa fursa kwa viongozi wa kamati za ulinzi na usalama kuelewa vyema majukumu yao na kuhakikisha kuwa wanazingatia haki na sheria kwa manufaa ya wananchi.
Aidha, aliishukuru Wizara ya Katiba na Sheria kwa kuandaa mafunzo ya Elimu ya Uraia na Utawala Bora, ambayo yanalenga kuwajengea uwezo watendaji wa kata, viongozi wa kamati za ulinzi na usalama, pamoja na viongozi mbalimbali kutoka wilaya hizo.
Mchatta aliongeza kuwa mafunzo hayo ni hatua muhimu ya Serikali katika kuboresha utawala bora na kuimarisha ushirikiano kati ya viongozi na wananchi.
Pia alisisitiza kuwa ushirikiano kati ya viongozi na wananchi ni msingi wa kuimarisha usalama na utulivu katika jamii.
Mafunzo haya ni sehemu ya juhudi endelevu za Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria katika kuhakikisha kuwa viongozi wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria na kuheshimu haki za raia.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.