Makamu wa Rais, Dkt.Philip Mpango ameeleza magonjwa yasiyoambukiza yanachangia vifo nchini kwa asilimia 33 ikiwemo kisukari na shinikizo la damu.
Ameeleza katika miaka ya 1980 ni asilimia moja tu ya watanzania waliokuwa wakisumbuliwa na ugonjwa wa kisukari na asilimia 5 ugonjwa wa shinikizo la damu.
Mpango amefafanua, kwasasa hali imebadilika ambapo kisukari kinaathiri watanzania kwa asilimia 25 na ugonjwa wa shinikizo la damu kwa asilimia 9.
Akizungumza katika maadhimisho ya miaka 50 ya kampeni ya mtu ni afya na uzinduzi wa mtu ni afya awamu ya pili, yenye kauli mbiu Mtu ni afya,Afya Yangu wajibu wangu, wilayani Kibaha mkoani Pwani, alisema wakati kampeni hii inazinduliwa wananchi wana wajibu wa kujikinga na maradhi.
Alihimiza wananchi kujikinga na maradhi,kufuata elimu zinazotolewa na wataalamu wa afya ili kupunguza mzigo mkubwa wa gharama za matibabu kwao wenyewe na Serikali.
Alisisitiza ujenzi usafi wa mazingira,ujenzi wa vyoo bora na kujiepusha kutupa taka ovyo kuanzia ngazi ya familia, kujenga tabia ya kunawa mikono kwa kutumia maji tiririka,kuchemsha maji kwa afya yao.
Pamoja na hayo Mpango alihimiza hedhi salama kwa wanafunzi na usafi kwenye mazingira ya shule, halmashauri,majiji na wilaya na kuondokana na kutupa taka ngumu, kujenga tabia ya kufanya mazoezi ya viungo ili kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza.
Kadhalika Mpango alikemea tabia ya uharibifu wa mazingira, kuchoma moto mashamba na kukata miti ovyo ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Alisisitiza matumizi ya nishati safi kwa kuachana na matumizi ya nishati hatarishi, ambayo ni kuacha matumizi ya mkaa na kuni ili kulinda afya ya .
Nae Waziri wa Afya Ummy Mwalimu alieleza, Serikali ilianza kuchukua hatua mbalimbali kudhibiti na kuboresha huduma za afya nchini na kupunguza ama kutokomeza baadhi ya magonjwa yasiyoambukiza baada ya Uhuru ambapo Serikali iliamua kupambana na adui maradhi, umaskini na ujinga.
Alisema mwaka 1973 ilizindua rasmi kampeni ya mtu afya kupambana na adui maradhi ambapo kuanzia kipindi hicho iliendelea kuzindua kampeni mbalimbali ikiwemo usichukulie poa Nyumba ni choo.
Ummy alieleza kupitia kampeni hii ya mtu ni afya awamu ya pili benki ya dunia imetoa bilioni 5.5 kwa ajili ya utekelezaji utakaotekelezwa kwa awamu kwa miaka saba.
Katika hatua nyingine,Ummy alitaja washindi wa usafi wa mazingira na matumizi ya vyoo bora na kukabiliana na magonjwa ya mlipuko, na kusema mkoa wa Iringa umeibuka kidedea nchini.
Katika halmashauri ya mji nchini imeshinda mji wa Njombe, halmashauri ya wilaya Njombe, halmashauri ya majiji ni Tanga,manisapaa imeshinda Shinyanga na kundi la vyuo vikuu imeshinda chuo kikuu cha Dar es Salaam.
Awali Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge alieleza kwa kipindi cha miaka mitatu mkoa huo umepokea fedha za miradi ya maendeleo, kiasi cha sh.trilioni 1.229.
Akielezea kuhusu uwekezaji alisema, mkoa una viwanda 1,553 kati ya hivyo 124 ni vikubwa ambapo tangu tangu Rais Samia Suluhu Hassan ainge madarakani miaka mitatu viwanda 34 vimejengwa na kati yake 19 vipo hatua mbalimbali za ujenzi.
Kunenge alieleza, mkoa umetenga maeneo ya viwanda na kuboresha mazingira na miundombinu mbalimbali ili kuvutia wawekezaji.
Vilevile alielezea, dkt Mpango kama mlezi alikuwa afurahishwi na matokeo ya kilimo cha biashara cha korosho, hivyo amemhakikishia kwamba,mkoa umejipanga kuendelea kutoa mchango mkubwa kwenye kilimo hicho na kuleta tija katika Taifa.
Kuhusu uharibifu wa mazingira,ambapo watu wamekuwa wakichoma moto ovyo mashamba,kukata miti, anasema, wanafanya operesheni na doria kudhibiti hali hiyo bila kuonea wala kuumiza mtu.
Kunenge alisema, hadi sasa kutokana na operesheni hizo wamekamata pikipiki 900 (busta)zinazobeba mkaa kinyume na utaratibu na watuhumiwa 79 ambao nao upelelezi unaendelea na watafikishwa mahakamani.
Kadhalika Mkuu huyo wa mkoa,alimpa pole Rais Samia kwa changamoto ya mafuriko iliyotokana na mvua ikiwemo mkoa wa Pwani katika wilaya ya Rufiji, Kibiti na Kisarawe sanjali na kimbunga Hidaya kule wilayani Mafia wakati.
Alielezea, kimbunga Hidaya Mafia kimeharibu nyumba 994, kwa Rufiji na Kibiti kambi za waathirika zipo nne ambapo tatu Kibiti na moja Rufiji.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.