Makamu wa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan, amesema serikali itafuatilia baadhi ya wafanyabiashara wanaodaiwa kuingiza bidhaa feki na kuuuza kwa gharama nafuu hali inayosababisha kushusha soko la ndani.
Hayo ameyasema wakati akizindua kiwanda cha African Dragon kinachotengeneza malighafi ya mabati, Zinga Wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani kilichojengwa kwa thamani ya bilioni 11 na alisema kuwa suala hilo amelichukua na kuahidi kulifanyiwa kazi.
Aidha alieleza kuwa, kwa hali hiyo inakatisha tamaa na jitihada za wawekezaji wa ndani katika juhudi za serikali kuhamasisha wawekezaji kuwekeza nchini.
Mhe.Samia alielezea ,sekta ya viwanda kwa sasa ndiyo mpango wa serikali wa kihakikisha nchi inakuwa kwenye uchumi wa kati kupitia viwanda.
“Ofisi yangu imelichukua suala hilo na italishughulikia “alisisitiza Samia.
Hata hivyo aliwaasa wazazi na walezi kusimamia vijana wao kupata elimu ya ujuzi wa kuweza kuajiriwa ili kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira.
Pia aliupongeza Mkoa wa Pwani kwa kuongoza kwa kusheheni viwanda kitaifa, amewaomba kujipanga na kuvutia wawekezaji katika mkoa, kwani sio kazi rahisi.
“Katika utekelezaji wa Uchumi wa viwanda ,mtoe ushirikiano kwa wawekezaji ili kuweza kutimiza malengo ya serikali ya kuelekea uchumi wa kati “alieleza Mh.. Samia.
Akimkaribisha makamu wa Rais, Mkuu wa mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo alisema Mkoa huo, una jumla ya viwanda 429 ikiwemo vya kati, vikubwa na vidogo ,na kutengeneza ajira za moja kwa moja zaidi ya 20,000 na kunufaika na ushuru na kodi inazolipa viwanda hivyo.
Mhandisi Ndikilo alieleza, moja ya changamoto ni ukosefu wa soko ambapo kwa Bagamoyo tayari viwanda viwili ikiwemo cha nguzo za zege za umeme kimefungwa na kiwanda cha viungo macho kimesimamisha uzalishaji.
Alieleza umeme uliopo ni megawatts 62 mahitaji ni 79 kimkoa, wanapengo la megawatts 17 ili kupata umeme wa kutosha .
Katika hatua nyingine nae Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Siling Soun alisema ,kilianzishwa 2015 ,kimegharimu bilioni 11 ikiwa ni gharama za mitambo na ujenzi.
Alisema, kwasasa wameshatoa ajira 50 za moja kwa moja na kulipa ushuru wa halmashauri milioni 30 mwezi june mwaka huu.
Soun alitaja changamoto zinazowakabili kuwa ni pamoja na kukatika kwa umeme na kusababisha hasara ya milioni mbili pamoja na soko kuwa sio la uhakika kutokana na uingizwaji wa bidhaa feki zinazonunuliwa na kuingizwa kutoka nje ya nchi na kuuzwa kwa gharama nafuu.
Alitaja ,changamoto nyingine ni miundombinu mibovu hali inayosababisha usafirishaji kuwa sio rafiki.
Akijibu changamoto za umeme, Naibu waziri wa nishati,Subira Mgalu alisema katika kutatua changamoto kiwandani hapo, wanatarajia kupunguza tatizo hilo kupitia ujenzi wa umeme kutoka Tegeta hadi eneo la uwekezaji (EPZA )Bagamoyo.
Alisema, kwenye masuala ya miundombinu ya umeme wameshaanza kutatua changamoto hizo kwa kuanzishwa miradi mikubwa ya umeme nchini ikiwemo stiglers gorge huko kwenye maporomoko ya mto Rufiji.
Samia yupo kwenye ziara ya kikazi ya siku sita mkoani Pwani, oktoba 24 alikuwa Bagamoyo na oktoba 25 ataendelea Bagamoyo na Chalinze ambapo oktoba 29 itamalizika.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.