Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Selemani Jafo (Mb), leo amefungua rasmi Maonesho ya Biashara na Uwekezaji yanayoendelea mkoani Pwani na kutoa agizo la kuyafanya maonesho hayo kuwa ya kitaifa kila mwaka. Mhe. Jafo amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil T. Abdallah, kuhakikisha maonesho haya yanapandishwa hadhi na kusimamiwa kwa kushirikiana na Mkoa wa Pwani.
“Sasa namuagiza Katibu Mkuu wa Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil, kuanzia sasa maonesho haya ya viwanda, biashara, na uwekezaji yawe ya kitaifa. Yasimamiwe na Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Mkoa wa Pwani, na kila mwaka yafanyike hapa Pwani,” alisema Mhe. Jafo.
Aidha, Waziri Jafo alibainisha kuwa Mkoa wa Pwani kwa sasa ni kinara wa uwekezaji wa viwanda nchini, hivyo ni muhimu kuupa heshima kwa kuyafanya maonesho hayo kuwa ya kitaifa. Alisifu juhudi za uongozi wa Mkoa wa Pwani katika kuhakikisha mazingira rafiki kwa wawekezaji, hali inayochangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa sekta ya viwanda nchini.
Mhe. Jafo pia alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuimarisha mazingira wezeshi kwa wawekezaji. Alifafanua kuwa tangu mwaka 2021, idadi ya viwanda nchini imeongezeka kutoka viwanda 52,000 hadi zaidi ya viwanda 80,000, ikiwa ni ongezeko la viwanda 28,000. Alitoa pongezi maalum kwa Mkoa wa Pwani kwa kuchangia kwa kiasi kikubwa ongezeko hilo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge, alitoa shukrani kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada za kukuza sekta ya viwanda na uwekezaji kupitia sera wezeshi. Alisema Mkoa wa Pwani umetafsiri sera hizo kwa vitendo kwa kuimarisha mazingira ya uwekezaji.
Mhe. Kunenge aliongeza kuwa serikali inaendelea kuboresha miundombinu kama vile umeme, barabara, maji, na masoko ili kuwezesha zaidi uwekezaji. Alibainisha kuwa katika sekta ya umeme, Mkoa wa Pwani umeongeza uzalishaji wa megawati 19, hatua inayochochea maendeleo ya viwanda.
Maonesho haya yanatarajiwa kuwa chachu ya kukuza biashara, uwekezaji, na uchumi wa Taifa kwa ujumla.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.