Mkuu wa Mkoa wa Pwani ambaye pia ni Mwenyekiti wa Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki, Mhe. Abubakar Kunenge, amesema Maonesho ya mwaka huu ni ya kipekee kwa kuwa yameonyesha kwa vitendo utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa pamoja na Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) hususan katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi.
Mhe. Kunenge ameyasema hayo leo, Agosti 2, 2025, akitoa salumu za Mkoa wa Dare salaam, Pwani na Tanga wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki yanayofanyika katika Viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mkoani Morogoro.
Ameeleza kuwa maonesho haya yanaakisi utekelezaji wa vipaumbele vya Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuongeza tija na ufanisi kwa wananchi kupitia sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi. Aidha, amebainisha kuwa Serikali inaendelea kuboresha miundombinu na kuhamasisha matumizi ya teknolojia za kisasa kwa ajili ya kilimo chenye tija.
Akitoa mfano, Mhe. Kunenge amesema uzinduzi wa Reli ya Kisasa ya Mizigo (SGR) uliofanyika Julai 31, 2025 kule Kwala, mkoani Pwani na kuongozwa na Mhe. Rais, ni fursa muhimu kwa wakulima kwani utarahisisha usafirishaji wa mazao kwa ufanisi mkubwa, jambo ambalo ni kipaumbele cha Serikali katika kuimarisha uchumi wa kilimo.
Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki yanajumuisha mikoa minne ambayo ni Dar es Salaam, Pwani, Morogoro na Tanga, huku yakiendeshwa chini ya kaulimbiu isemayo: “Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.”
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.