Serikali Mkoani Pwani kwa kushirikiana na mradi wa Shule Bora inaendesha mafunzo ya kusimamia na kutekeleza mtaala wa somo la Hisabati elimu ya Msingi ili kuongeza ufaulu wa somo hilo.
Akifungua mafunzo hayo katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Minaki Wilayani Kisarawe Katibu Tawala Mkoa wa Pwani ambaye pia ni Skauti Mkuu, Rashid Mchatta aliyewakilishwa na Afisa Elimu Mkoa huo Sarah Mlaki amesisitiza walimu kutumia ufanisi, umahiri na zana stahiki kupitia mbinu za ufundishaji wa somo hilo.
"Kumekuwa na changamoto kwa baadhi ya wanafunzi kwenye somo la hisabati ambapo utafiti umebaini baadhi yao hufanya vibaya kwenye mitihani ya Taifa ikiwemo ile ya kujipima "Mock" Wilaya na Mkoa," amesema Mchata.
Naye mtaalamu kiongozi wa Shule Bora Vicent Katabalo amupongeza Mkoa wa Pwani kwa jitihada zake za kusimamia vyema mipango na miradi mbalimbali ya Serikali ikiwemo ya kuinua kiwango cha elimu na kuwa Mkoa huo ni wa kimkakati kwani ndiyo kiongozi wa mikoa mingine tisa yenye mradi wa shule bora na unabeba maendeleo ya nchi.
Kwa upande wake ofisa elimu mkoa wa Pwani Sara Mlaki amesema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuimarisha umahiri wa wa walimu na viongozi wa Elimu katika kutumia mbinu shirikishi za ufundishaji na ujifunzaji wa somo la Hisabati ili kuleta matokeo chanya kwa wanafunzi wote.
Mafunzo hayo ambayo ni endelevu ya walimu kazini (MEWAKA) kuhusu moduli iliyoboreshwa kulingana na rasimu ya mtaala mpya wa elimu ya msingi yameandaliwa na Ofisi ya Rais (TAMISEMI) kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia pamoja na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kupitia Program ya Shule Bora ambayo inatekelezwa katika mikoa tisa ya Tanzania Bara kwa Ufadhili wa Serikali ya Uingereza na kwa Usimamizi wa Cambridge Education.
Wawezeshaji wa mafunzo hayo wanatoka kwenye vyuo vya Ualimu vya Tukuyu na Mpwapwa ambapo washiriki wa mafunzo hayo ni viongozi wa Elimu kutoka katika ngazi ya Mkoa wakiwemo Walimu, Walimu wakuu, Maofisa Elimu Kata, Maafisa Elimu Awali na Msingi kutoka katika Halmashauri tisa na shule teule za Wilaya ya Kisarawe.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.