Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, ametangaza kuwa mkoa huo utakuwa mwenyeji wa uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2025. Hafla hiyo itafanyika tarehe 2 Aprili 2025 katika viwanja vya Shirika la Elimu Kibaha.
Kunenge alitoa taarifa hiyo leo 28 Aprili wakati wa kikao na waandishi wa habari kilichofanyika ofisini kwake, Kibaha Mjini. Alibainisha kuwa maandalizi yanaendelea vizuri na akawahimiza wadau na wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika tukio hilo muhimu la kitaifa.
Akimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Kunenge alisema kuwa heshima kubwa imetolewa kwa Mkoa wa Pwani kwa kuchaguliwa kuwa mwenyeji wa uzinduzi huo. Alisema Rais Samia alitangaza uamuzi huo wakati wa kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa na kumbukumbu ya Hayati Mwalimu Julius Nyerere mnamo Oktoba 14, 2024, jijini Mwanza.
Rais Samia alitangaza kuwa mwaka 2025 Mwenge wa Uhuru utawashwa Pwani. Serikali na wananchi tumepokea kwa heshima kubwa, na sasa tunaendelea na maandalizi ya mwisho, alisema Kunenge.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa alibainisha kuwa hafla hiyo itawahusisha viongozi wa kitaifa, wageni kutoka ndani na nje ya nchi, huku ikiambatana na burudani mbalimbali. Pia, Mwenge wa Uhuru utapita katika halmashauri tisa za Mkoa wa Pwani kwa ajili ya kuzindua na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi ya maendeleo.
Kunenge alihimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika fursa za kiuchumi na kibiashara zitakazopatikana wakati wa mbio za Mwenge huo. Aliongeza kuwa viwanja vya Shirika la Elimu Kibaha vilichaguliwa kwa uzinduzi huo kwa kuwa ni eneo linalofikika kirahisi, na maandalizi yote yamepangwa kwa umakini kuhakikisha tukio linafanikiwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.