Mbio za Mwenge wa Uhuru 2023 zinatarajia kukagua, kuweka mawe ya msingi, kuzindua na kufungua jumla ya Miradi 99 ya maendeleo yenye thamani ya sh. trilioni 4.4 mkoani Pwani.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge ametoa taarifa hiyo leo Mei 15, 2023 alipokabidhiwa Mwenge wa Uhuru na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Fatma Mwassa, eneo la Ubena Halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo.
Kunenge amesema Mwenge wa uhuru utakimbizwa zaidi ya kilomita 1000 kukagua miradi mbalimbali katika Wilaya saba na Halmashauri tisa za Mkoa wa Pwani ambapo kati ya miradi hiyo 99, tisa itafunguliwa, 15 itazinduliwa,20 itawekewa mawe ya msingi na 55 itakaguliwa.
Ameongeza kuwa Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2023 yenye kauli mbiu isemayo "Tunza mazingira, okoa vyanzo vya Maji kwa ustawi wa viumbe hai," itasaidia kulinda na kutunza mazingira na kuufanya mkoa huo kuendelea kuwa wa kijani.
“Katika kuunga mkono jitihada za Serikali kutunza mazingira, hadi kufikia mwezi Aprili mwaka 2023 Mkoa wa Pwani umepanda miti milioni saba sawa na asilimia 57.5 katika maeneo mbalimbali, lengo letu ni kupanda miti milioni 13 kwa mwaka huu,” amesema Kunenge na akaongeza kuwa hatua hiyo inalenga uboreshaji wa mazingira na kutekeleza matakwa ya sheria ya mazingira ya mwaka 2004 ambayo yanataka shughuli zote zinazofanyika zizingatie tathmini ya athari za mazingira.
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa amesema tayari mikakati mbalimbali ya utunzaji mazingira imefanyika ikiwemo, kufanya doria kuzuia uharibifu wa vyanzo vya maji vinavyotokana na shughuli za kibinadamu kilimo, ufugaji na uchomaji miti hovyo, uhamasishaji na utoaji wa elimu juu ya umuhimu wa kutunza mazingira na kuzindua kampeni ya matumizi ya nishati mbadala ambayo yatazalisha fursa nyingi za kiuchumi
Mbio za Mwenge wa uhuru mwaka 2023 zinakimbizwa na timu ya watu sita wakiongozwa na Abdallah Shaibu Kaim na unatarajiwa kuhitimishwa Octoba 14 mwaka huu mkoani Manyara.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.