Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, ambaye pia ni Skauti Mkuu wa Tanzania, Rashid Mchatta, ameagiza Idara ya Uzalishaji kushirikiana na wasimamizi wa Mradi wa Kutunza Mazingira unaosimamiwa na Jane Goodall Institute Tanzania kupitia Mradi wa COSME. Lengo kuu ni kuandaa muundo wa utekelezaji wa mradi huo ambao utajumuisha viongozi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wake.
Mchatta alitoa maelekezo hayo leo katika kikao cha kimkakati kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya taasisi za serikali na wadau wa mradi ili kuhakikisha jitihada za kuhifadhi mazingira zinafanikiwa, sambamba na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, pamoja na kuinua uchumi wa kaya na kuimarisha usawa wa kijinsia.
Kwa upande wake, Meneja wa Mradi huo, Dkt. Namkunda Johnson, alibainisha kuwa mradi unalenga kuhifadhi mazingira kwa kutumia mbinu mbalimbali kama uanzishwaji wa vitalu vya kupanda miti katika vijiji, uundaji wa vikundi vya kuweka na kukopeshana (COCOBA), na kuanzisha misitu ya kijiji. Aidha, Dkt. Namkunda aliongeza kuwa mradi utatoa elimu na kuhamasisha umma kupitia klabu za mazingira mashuleni zinazojulikana kama "Roots and Shoots," vikundi vya vijana, na kuanzisha mipango rasmi ya usimamizi wa misitu.
Pia, mradi utaimarisha uwezo wa kamati za maliasili za vijiji ili ziweze kusimamia na kulinda misitu ya vijiji kwa ufanisi zaidi, na hivyo kuhakikisha mazingira yanalindwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.