Waziriwa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa - TAMISEMI Mohamed Mchengerwa amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo na Mtendaji Mkuu wa Mtandao wa Barabara za Vijijini na Mijini - TARURA kuandaa mpango wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami ili zijengwe kwa asilimia 85 kufikia 2025.
Amesema Chama Cha Mapinduzi kilitoa ahadi ya kujenga barabara kwa kiwango cha lami na teknolojia mbadala kwa asilimia 85 hivyo utekelezaji huo unatakiwa kufanyika kwa maeneo ambayo bado hayajafikiwa.
"Mpango huu unifikie mara moja bila kujali gharama ni sh. ngapi nileteeni nikishapata tunajipanga sasa kwenda kutafuta fedha kumuomba Mh. Rais atupatie fedha ujenzi wa barabara zote nchi nzima katika mikoa yote 26 na wilaya zote," amesema na akaongeza "Maana yake ni kuwa Mhe. Rais na Ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2020-2025 inatutaka kujenga barabara zote kwa kiwango kizuri, ifikapo 2025 tufikie asilimia 85 tutafanya maamuzi zipi tuzianze."
Mchengerwa ametoa maelekezo hayo leo Disemba 1, 2023 katika Kijiji cha Mohoro alipohudhuria na kushuhudia hafla ya utiaji saini pamoja na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa daraja la Bibi Titi Mohamed kijijini hapo.
Akizungumzia umuhimu wa daraja la Bibi Titi Mohamed Mohoro, Mchengerwa amesema litakwenda kuondoa vifo vya wananchi vilivyokuwa vikitokea kipindi cha mvua wakati wananchi wakivuka katika daraja la awali.
Vilevile ameeleza kwamba kilio cha ujenzi wa daraja hilo ni cha muda mrefu na sasa wakazi wa vijiji vya Mohoro na Chumbi ambavyo kuna wakazi zaidi ya 60,000 hali zao za kiuchumi zitakwenda kuimarika.
"Kabla ya daraja hili hali za wananchi zilidumaa kutokana na kushindwa kusafirisha bidhaa wanazozalisha, wanafunzi kukwama kwenda shule kipindi cha mvua lakini pia mafuriko yaliyokuwa yanatokea yalisababisha vifo," ameeleza.
Ametoa pia maelekezo kwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge na Wataalamu wa TARURA Mkoa wa Pwani na Wilaya ya Rufiji kuhakikisha wanasimamia kwa weledi mradi huo ili ukamilike kwa ufanisi na kwa wakati uliopangwa.
Ameishukuru Serikali kwa kuongeza bajeti ya TARURA kutoka milion 502.5 kwa mwaka wa fedha 2021/2022 hadi kufikia zaidi ya Bilioni 7 kwa mwaka wa fedha 2023/ 2024 ambapo kati ya fedha hizo, tayari daraja hilo limetengewa sh. Biln 4 kuanza ujenzi.
Akimkaribisha Waziri Mchengerwa kuzungumza na wananchi, Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge ameishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa fedha za miradi ya maendeleo inayoondoa changamoto za wananchi.
Kunenge amesema katika kipindi cha uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, mkoa huo umepokea sh. Trilion 1.19 za miradi ya Maendeleo kati ya hizo sh. Bilioni 102.1 ni za Miundombinu ya barabara kwa Wakala wa Barabara TANROADS na TARURA.
Ameeleza kwamba kati ya fedha hizo za miundombinu fedha za TARURA ni sh. Bilioni 49.3 na kwamba kitendo cha Serikali kutoa zaidi ya sh. Bilini 11 kwa ujenzi wa daraja hilo unakwenda kufungua uchumi katika eneo hilo ambalo limekuwa kikwazo cha usafiri hususani kipindi cha mvua.
Ameahidi usimamizi wa kiwango cha juu utakaowezesha daraja hilo kukamilika kwa wakati huku akisema hakuna kikwazo kitakachokwamisha ujenzi wa daraja hilo.
Nae Mtendaji Mkuu wa TARURA Mhandisi Victor Seff amesema daraja hilo hadi kukamilika litagharimu sh. Bilioni 11.5 na kwamba litakuwa na urefu wa Mita 80 na kwamba litajengwa kwa miezi 18.
Pia amesema daraja hilo ambalo litajengwa kwa fedha za ndani likikamilika litadumu kwa miaka 100, litakuwa na makaravati mawili na barabara unganishi zenye urefu wa Km moja.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.