Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Mhandisi Evarist Ndikilo ameziagiza Halmashauri zote zilizoko katika Mkoa wa Pwani ziondoe udhaifu katika ofisi za wakaguzi wa ndani ili halmashauri hizo ziweze kuondokana na tatizo la kupata hati chafu.
Mhe. Ndikilo ametoa agizo hilo huko Mlandizi Wilayani Kibaha wakati wa kikao maalum cha baraza la Madiwani cha kujadili ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2016/17 ambapo Halmashauri hiyo imepata hati safi licha ya kuwa na hoja 18 ambazo zilikuwa hazijafungwa.
Kadhalika Mhe. Mkuu wa Mkoa amezitaka Halmashauri zote za Mkoa wa Pwani kuondokana na utunzaji hafifu wa kumbukumbu na nyaraka muhimu zinazotumika wakati wa manunuzi kwani hali hiyo pia husababisha Halmashauri nyingi kukosa vielelezo vya namna fedha zilivyotumika na hivyo kuleta hoja kwenye ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali.
Kwa upande wao Madiwani pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Bibi Tatu Selemani wamelia na changamoto ya upungufu wa watumishi na kumuomba Mkuu wa Mkoa kusaidia ili Halmashauri iweze kupata kibali cha kuajiri wafanyakazi ili kuziba mapengo yaliyoachwa na watumishi walioondoshwa kwa vyeti ya kughushi
Akitolea ufafanuzi wa tatizo la upungufu wa wafanyakazi katika Halmashauri hiyo Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Ndg. Zuberi Samataba amesema tayari Serikali imeanza kutoa vibali vya kuajiri lakini akawataka watumishi walioko maofisini kufanya kazi kwa juhudi wakati Serikali ikiendelea na zoezi la kuajiri watumishi wapya na wenye sifa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.