Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah, ameongoza maadhimisho ya miaka 10 ya kuanzishwa kwa Kiwanda cha Tanzania Biotech Products Limited (TBPL) kilichopo Kibaha, mkoani Pwani. Hafla ya uzinduzi wa maadhimisho hayo imefanyika Oktoba 16, 2025, katika eneo la kiwanda hicho.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Abdallah alisema kuwa TBPL ni nguzo muhimu katika maendeleo ya sekta za kilimo na afya nchini, kutokana na uwezo wake wa kuzalisha bidhaa za kibayolojia kama vile viuatilifu vya kupambana na mbu na wadudu waharibifu wa mazao.
Amesisitiza kuwa kiwanda hicho kimechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa kupitia uzalishaji wa ndani unaozingatia uhifadhi wa mazingira na kulinda afya za wananchi.
Aidha, Dkt. Abdallah alieleza kuwa TBPL imekuwa na mchango mkubwa katika kutoa ajira kwa Watanzania, kuendeleza ujuzi wa kitaalamu na kukuza ubunifu katika sekta ya viwanda vya kibayoteknolojia nchini.
Mafanikio hayo, alisema, yanaendana na Dira ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambayo inalenga kuimarisha viwanda vinavyotumia teknolojia na ubunifu wa ndani ili kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na kuboresha afya za wananchi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.