Mwenge wa Uhuru umeendelea na Mbio zake Wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani, ambapo umezindua na kukagua jumla ya miradi sita yenye thamani ya shilingi milioni 747.5, ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali katika kuimarisha maendeleo ya jamii kupitia sekta mbalimbali.
Miongoni mwa miradi hiyo ni uzinduzi wa boti ya doria na ukaguzi baharini katika soko la samaki, mradi wenye thamani ya milioni 40.603. Mradi huu unalenga kudhibiti upotevu wa mapato yatokanayo na uvuvi, kuzuia uvuvi haramu na biashara za magendo baharini, pamoja na kuimarisha usimamizi wa raslimali za uvuvi.
Mradi mwingine uliozinduliwa ni wa ununuzi wa gari na vifaa vya uzoaji taka kwa kikundi cha vijana cha SAFISHA Mazingira, kilichopo kata ya Nianjema, uliogharimu shilingi milioni 150.600. Lengo ni kuboresha usafi wa mazingira na kuwajengea vijana uwezo wa kujiajiri.
Pia, Mwenge wa Uhuru uliweka jiwe la msingi katika mradi wa upanuzi wa tanki la maji Kidomole, mradi ulioanzishwa mwaka 2024 na kugharimu shilingi milioni 334.240. Mradi huu umetekelezwa kupitia mfumo wa kielektroniki wa manunuzi (NeST) na unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi.
Aidha, jiwe la msingi liliwekwa katika mradi wa ujenzi wa boksi na kalvati barabara ya Kimalang’ombe - Makofia, wenye thamani ya shilingi milioni 121.951, unaotekelezwa na TARURA, kwa lengo la kuboresha miundombinu ya usafiri na usafirishaji katika maeneo ya vijijini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa miradi hiyo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, Ismail Ali Ussi, alisema ameridhishwa na utekelezaji wa miradi hiyo na kuagiza wahusika kuitunza na kuisimamia ipasavyo ili ilete tija kwa sasa na vizazi vijavyo. Alisisitiza kuwa serikali inatumia fedha nyingi kuhakikisha utekelezaji wa miradi ya aina hiyo kwa manufaa ya wananchi.
Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Shaibu Ndemanga, alipokea Mwenge wa Uhuru tarehe 8 Aprili 2025 kutoka Wilaya ya Mafia, na kueleza kuwa katika mapokezi hayo, miradi sita imepitiwa ambapo mmoja umewekewa jiwe la msingi na mingine mitano kuzinduliwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.