Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda ametoa maagizo kwa Wazazi na walezi ambao wamekumbwa na mafuriko katika maeneo mbalimbali Wilayani Kibiti na Rufiji kuhakikisha watoto wao wanasoma shule zilizokaribu na maeneo waliyohamia.
Aidha amewaelekeza walimu kuwapokea wanafunzi waliotoka maeneo ya mafuriko bila masharti na kutoa taarifa kwa Maafisa elimu Ili kupata idadi kamili ya waliorudi shuleni.
Pro.Mkenda ametoa maagizo hayo April 22, 2024 alipokuwa katika ziara ya siku moja Wilaya ya Rufiji na Kibiti kukagua shule zilizoathirika na mafuriko, kutembelea makambi pamoja na kutoa vitabu na daftari kwa wanafunzi waliokumbwa na mafuriko
Amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha wanafunzi waliokuwa kwenye maeneo ya mafuriko wanaendelea na masomo popote walipo wakati taratibu nyingine zikiendelea za kuboresha miundombinu maeneo ambayo hayana mafuriko
" Mwanafunzi akija kwenye shule yako mpokee mengine yatatatuliwa baadae haya ni maelekezo walimu wote wayasikie, Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza tuongezee nguvu kuhakikisha wanafunzi kwenye maeneo yaliyoathiriwa wanaendelea na masomo," amesema.
Mkuu wa Mkoa wa PWANI Abubakar Kunenge amesema katika maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko watazungumza na wananchi na maamuzi ya Serikali yatafanyika kunusuru maisha yao kwa kuhamia sehemu salama.
Kunenge amesema baada ya mafuriko kipaumbele kiliwekwa kwa wanafunzi ambao wanatarajiwa kufanya mitihani mwaka huu na kutafutiwa shule kwa haraka na sasa wanafunzi wengine wanaendelea kurejea mashuleni kwenye maeneo ambayo wanaishi.
Afisa elimu Mkoa wa Pwani Sara Mlaki ameeleza kwamba katika Wilaya ya Rufiji wanafunzi 7,264 wameathiriwa na mafuriko huku Wilaya ya Kibiti wanafunzi 824 wakikumbwa na adha hiyo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.