Mkoa wa Pwani umesaini makubaliano ya pamoja na Kampuni ya Magazeti ya Serikali, Tanzania Standard Newspapers (TSN) kuratibu na kusimamia maonesho ya Viwanda na Biashara yaliyopangwa kuanza Oktoba 1 hadi 7 Mwaka huu kwenye uwanja wa CCM ujulikanao kama Sabasaba Mkuza-Kibaha.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye hafla ya kusaini makubaliano hayo, Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo ameelezea malengo ya maonesho hayo aliyoyataja kama “kubwa kuliko” kuwa ni kutanabaisha wana Pwani, watanzania na Dunia kuhusu hatua ambayo mkoa umefikia katika ujenzi wa Viwanda, kuwezesha wenye viwanda kupata Masoko ya bidhaa kwa kuwakutanisha na wanunuzi ikiwa ni pamoja na kuvutia wawekezaji wapya.
“Malengo ya Kongamano la uwekezaji ni kuonesha fursa za uwekezaji zilizopo kwenye Sekta mbalimbali kama Kilimo, Mifuko, Uvuvi, utalii na kwenye huduma zingine” alisema mhandisi Ndikilo.
Mbali na TSN na TANTRADE, Mhandisi Ndikilo aliwataja wadau wengine kuwa ni waonesha bidhaa mbalimbali, taasisi wezeshi ambazo alitaja baadhi kuwa ni TIC, Brela, TBS, NIDA, NSSF, NEMC, TRA, SIDO, Zimamoto na TANESCO, viongozi wa kitaifa na wa serikali, Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara za kisekta.
Wadau wengine waliotajwa ni Wawakilishi wa mashirika ya kimataifa, mabalozi Wanaowakilisha mataifa yao hapa nchini, viongozi wa Mikoa jirani na taasisi zingine mbalimbali pamoja na wananchi ambao ametumia fursa hiyo kuwahamasisha kufika na kupata taarifa za upatikanaji wa bidhaa mbalimbali za viwandani.
Makubaliano hayo yalisainiwa katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani ambapo Mkoa uliwakilishwa na Katibu Tawala Mkoa Theresia Mhando na TSN iliwakilishwa na Afisa Masoko na Mauzo Januarius Maganga.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.